Tanesco yatoa sababu Kagera kutumia umeme wa Uganda

Thursday August 22 2019

Wataalamu wa Tanesco,Wizara ya Nishati ,Gridi ya Taifa ya Uganda,Tanesco,,Mkoa wa Kagera,mwananchi habari, gazeti la mwananchi, siasa, uchaguzi wa serikali za mitaa, uchaguzi mkuu wa Tanzania,

 

By Aurea Senmtowe, Mwananchi

Dar es Salaam.  Huenda ukawa unajiuliza ni kwa sababu gani mkoa wa Kagera unatumia umeme kutoka nchini Uganda na siyo ule wa gridi ya taifa kama mikoa mingine.

Ukweli ni kuwa kutokana na umbali kutoka kwenye vyanzo vya ufuaji umeme ulifanya gharama za usafirishaji kwenda katika mkoa huo kuwa kubwa kuliko kutumia ule unaotoka Uganda.

Kagera ni miongoni mwa mikoa minne ambayo bado haijaunganishwa katika gridi ya taifa ambapo mingine ni Kigoma, Katavi pamoja na Rukwa.

Hayo yamebainishwa katika taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Agosti 22,2019 na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupitia ofisi ya uhusiano makao makuu iliyolenga kubainisha ni kwa nini mkoa huo ulikosa umeme kwa siku tatu.

Kukatika kwa umeme huo kulitokana na mti wa Caristus kuangukia nguzo za umeme mkubwa nchini Uganda na kukata waya katika njia ya umeme inayotoka Masaka kuelekea Kagera Tanzania.

Katika sehemu ya taarifa hiyo inaeleza wakati Kagera ikiunganishwa na umeme kutoka Uganda, nchini Tanzania vyanzo vikuu vya kufua umeme vilikuwa ni Nyumba ya Mungu (Kilimanjaro), Hale (Tanga), Mtera(Dodoma), Kidatu(Morogoro) ambao ulipekwa maeneo mbalimbali.

Advertisement

“Lakini hadi kufikia miaka ya 1990 baadhi ya maeneo ya nchi yalikuwa bado hayajaunganishwa na gridi ya taifa, kutokana na umbali kutoka vyanzo vya ufuaji umeme na gharama ambazo zingetumika.”

“Hivyo taifa lililazimika kufanya miradi mbadala kwa ajili ya kufikisha umeme wa uhakika katika maeneo ambayo yalikuwa hayajafikiwa ikibidi kutoka nchi jirani kwa ajili ya mikoa iliyo mbali, pia pembezoni mwa nchini ikiwemo Kagera,” imeeleza taarifa hiyo

Pia, taarifa hiyo inaeleza hadi kufikia mwaka 1992 Kagera iliunganishwa katika gridi ya taifa ya Uganda kupitia njia kuu ya umeme msongo wa 132 kV kutoka Masaka Uganda kwenda Kyaka Tanzania kujengwa.

“Jitihada zinaendelea kuhakikisha mkoa wote wa Kagera unapata umeme kupitia gridi ya taifa Tanzania kama ilivyo kwa wilaya za Muleba, Ngara na Biharamulo. Suala hili litafanyika mara baada wa Rusumo kukamilika,” inaeleza sehemu ya Taarifa

 

 


Advertisement