VIDEO: Tanga, Katavi na Ruvuma kutofanya uchaguzi Serikali za mitaa

Muktasari:

Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) nchini Tanzania, Seleman Jafo amesema mikoa ya Ruvuma, Katavi na Tanga hakutafanyika uchaguzi wa Serikali za mitaa kutokana na wagombea wa vyama mbalimbali kupita bila kupingwa.

 


Dodoma. Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) nchini Tanzania, Seleman Jafo amesema mikoa ya Ruvuma, Katavi na Tanga hakutafanyika uchaguzi wa Serikali za mitaa kutokana na wagombea wa vyama mbalimbali kupita bila kupingwa.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Novemba 23, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma akibainisha kuwa Novemba 25, 2019 ndio atatoa takwimu za idadi ya wagombea na vyama vyao walioshiriki uchaguzi huo unaofanyika kesho Jumapili Novemba 24, 2019.

Amesema katika mikoa hiyo, wagombea katika vijiji, mitaa, vitongoji  na  wajumbe walipita bila kupinga. Alipoulizwa ni wagombea wa vyama gani waliopita bila kupingwa katika mikoa hiyo, waziri huyo wa Tamisemi hakuliweka hilo wazi, kuahidi kutoa ufafanuzi Jumatatu.

Jafo amesema vyama  vilivyoandika barua ya kujitoa vinapaswa kutambua kuwa wagombea wake ndio wanaopaswa kuandika barua hizo ili kuondolewa katika mchakato wa uchaguzi.

Vyama ambavyo havitashiriki uchaguzi huo ni Chadema, UPDP, CUF, NCCR-Mageuzi na ACT-Wazalendo.

"Baada ya kutangaza kujitoa, nilitoa maelekezo kwa vyama kwa mujibu wa ibara ya 19 na 20 ya kanuni za uchaguzi kuwa wagombea walipaswa kuandika barua za kujitoa sasa kama hawakufanya hivyo watakuwa hawajajitoa,” amesema Jafo.

Amewataka wagombea kumaliza kampeni zao leo, kuwakumbusha wapambe wao kutovaa sare za vyama wakati wa kupigakura.