Tanzania kuanza upasuaji wa ubongo bila kufumua fuvu

Friday November 22 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imetenga Sh7.9 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya upasuaji wa ubongo katika Taasisi ya Mifupa (MOI), ikikamilika wagonjwa wataanza kukufanyiwa upasuaji wa ubongo bila kufumuliwa fuvu.

Mashine itakayotumika katika upasuaji huo ya ‘Angio Suite’ imeshanunuliwa na itawasili nchini Desemba, 2019.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Novemba 22, 2019 na mkurugenzi mtendaji wa MOI, Dk Respicious Boniface wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya miaka minne ya taasisi hiyo tangu Rais wa Tanzania, John Magufuli alipoapishwa kuwa kiongozi mkuu wa nchi Novemba 5, 2015.

Dk Respicious amesema Serikali ilitoa fedha hizo Mei, 2019 na tayari taratibu zote zimekamilika ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu nchini China.

“Serikali imetoa Sh7.9 bilioni kujenga maabara ya kisasa ya upasuaji wa ubongo. Maabara hii itaiwezesha taasisi kufanya upasuaji wa matatizo ya mishipa ya damu kichwani pasipo kulazimika kufungua fuvu la kichwa.”

"Mashine hii itakua na uwezo wa kutibu damu iliyoganda kwenye mishipa ya damu miguuni. Uwepo wa maabara utaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi chache Afrika zinazotoa huduma hiyo. Tunatarajia kuanza huduma Januari 2020,” amesema Dk Respicious.

Advertisement

Advertisement