VIDEO: Tanzania kufaidika na mpango wa viwanda wa SADC

Muktasari:

 Mpango wa Tanzania wa kukuza uchumi wa viwanda umeangaziwa katika mkakati wa viwanda wa mwaka 2015-2063 unaolenga katika mchakati, mikakati na program zenye lengo la kuendeleza ushindani katika uzalishaji.

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikielekea kwenye ukuaji wa uchumi wa kati utakaokuwa maendeleo ya viwanda, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imeweka mikakati ya kuziewezesha nchi wanachama kufikia malengo hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Agosti 12,2019 jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, Mkurugenzi wa maendeleo ya viwanda na Biashara wa SADC, Calicious Tutalife amesema ili kufikia maendeleo ya viwanda kwa nchi wanachama, jumuiya hiyo inatekeleza mkakati wa viwanda wa mwaka 2015/2063 unaolenga katika mchakato, mikakati na programu zenye lengo la kuendeleza ushindani katika uzalishaji.

“Mkataba wa viwanda ulipitishwa baada ya kupitiwa na kuongezewa mambo mbalimbali na vyombo vya jumuiya na rasimu yake ilipelekwa kwenye kikosi kazi cha Baraza la Mawaziri Juni 2019. Ukishapitishwa utakuwa ndiyo chombo pekee cha utekelezaji wa maendeleo ya viwanda utakaofuata viwango vya kimataifa,” amesema Tutalife.

Amesema tayari wajumbe kutoka nchi wanachama wameshapewa semina wezeshi iliyofanyika Mchi 2019 nchini Afrika Kusini ambapo nchi za Botswana, Lesotho, Eswatini, Malawi, Mozambique, Namibia, Tanzania na Zambia zinazofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la ushirikiano la Ujerumani (GIZ) zilishiriki.

Kuhusu biashara, Tutalife amesema mpaka Machi 2019 nchi wanachama wa SADC walimaliza awali ya kwanza ya majadiliano ambapo mambo manne kati ya sita yalikubaliwa.

Ametaja mambo yaliyokubaliwa ni pamoja na mawasiliano, fedha, utalii na usafirishaji, huku mambo mawili ambayo ni ujenzi na nishati yaliwekwa kiporo hadi utakapofanyika mkutano wa 39 wa Jukwaa la Biashara (TNF) utakaofanyika katika kipindi cha mwaka 2019/20.