Tanzania kutumia Tehama, kampuni za simu kutoa ushauri wa kilimo

Muktasari:

  • Tanzania ina uhaba wa maofisa ugani takribani 12,000 jambo lililoifanya Serikali kuwageukia wataalamu wa Tehama kutumia simu kutoa ushauri wa kilimo.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeanza kufanya mazungumzo na wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na kampuni za simu ili kuziba pengo la uhaba wa maofisa ugani takribani 12,000 nchini.

Akizungumza jana Jumanne Agosti 20, 2019  jijini Dar es Salaam katika mkutano ulioandaliwa na Jukwaa Huru la Kilimo (Ansaf), mkurugenzi msaidizi wa idara ya mafunzo huduma za ugani na utafiti ya Wizara ya Kilimo, Dk Kisa Kajiligi amesema kuna uhaba wa maofisa ugani takribani 12,000.

 “Tanzania tuna uhaba wa maofisa ugani licha ya kuwa na vijiji 12,545 lakini mabwana shamba tulionao ni 8,323 na  mahitaji kamili ni karibu 20,000.”

“Tumekutana na wadau wa Tehama na kampuni za simu ili kuangalia uwezekano wa kutumia simu za mkononi kupeleka elimu kwa wakulima. Mkulima atapiga simu atauliza swali na atajibiwa swali lake ili kuongeza uzalishaji,” amesema Dk Kajigili. 

Miongoni mwa wataalamu wa Tehama katika kituo cha utafiti cha Tari Naliendele, Happy Daudi amesema kituo hicho kinatekeleza teknolojia inayoitwa Ushauri hotline.

“Mkulima anaweza kupata utaalamu wa kilimo kupitia simu ya mkononi ya kawaida. Tunampa namba maalum ambayo akipiga atapata utaalamu wa kilimo na upatikanaji wa masoko,” amesema Happy.

Amebainisha kuwa teknolojia hiyo ina changamoto ya kutumia namba ya Kenya ambayo itawawia vigumu watumiaji baada ya majaribio kuisha.  

Kwa upande wake, Bless Mgongolwa aliyeanzisha program ya Agrobot pia ameeleza uzoefu wake, kwamba walipata ufadhili kutoka ubalozi wa Denmark Tanzania na kupeleka teknolojia yao katika mikoa ya Morogoro, Iringa na Morogoro.

“Tulipata wakulima zaidi ya 8,000 ambapo wakulima 500 walikuwa tayari kulipia huduma. Kwa wiki Sh300, kwa mwezi1,000 na kwa mwezi Sh2,000 na wakuliwa tayari kulipia kwa miezi miwili,” amesema.

Ameongeza kuwa kwa sasa wanafanya mazungumzo na Wizara ya Kilimo kukuza teknolojia hiyo.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Esoko, Patrick Kiao amesema wamefanikiwa kuwafikia zaidi ya wakulima150,000 katika Mikoa 14 nchini.

“Tunatumia Tehama kuwapa mafunzo wakulima kupitia simu za kawaida na simu janja. Tunayo pia programu ya knowledge plus inayowawezesha wakulima kupata mafunzo kupitia video zikiwa na maelezo ya mazao mbalimbali,” amesema Kiao.