Tanzania kuzikutanisha nchi 29 za Afrika, Nordic

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza wakati wa Mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusiana na Mkutano wa mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi tano za Nordic utakaofanyika  Novemba hapa nchini. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa 18 wa mawaziri wa mambo ya nje katika nchi za Nordic na Afrika.

Dar es Salaam. Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 34 zikiwemo nchi tano za Nordic.

Nchi hizo ni Sweden, Norway, Finland, Denmark na Iceland.

Hii ni mara ya 18 tangu mikutano hiyo ianze kufanyika na kwa mara ya kwanza mwaka 2019 Tanzania inakuwa mwenyeji ambapo mkutano huo unatarajiwa kufanyika Novemba 7 na 8, 2019  jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema jumla ya nchi 29 za Afrika zitashiriki mkutano huo.

Amesema takribani wageni 250 wanatarajiwa kushiriki kwenye mkutano huo kati yao wakiwemo mawaziri wa mambo ya nje 34.

Profesa Kabudi amesema lengo la mkutano huo ni kutoa nafasi kwa nchi za Nordic na nchi marafiki za Afrika kujadiliana kuhusu masuala ya ushirikiano kati ya pande hizo.

Sababu nyingine ni kuainisha vipaumbele katika ushirikiano huo pamoja na kuweka mikakati ya kutekeleza vipaumbele hivyo.

“Kwa mwaka huu mkutano utajadili namna ya kuimarisha mahusiano yenye tija kwa maendeleo ya nchi washiriki hususani kwenye sekta ya biashara na uwekezaji kwa maendeleo. Kingine ni ushirikiano kwenye masuala ya ulinzi na usalama,” amesema Profesa Kabudi.