VIDEO: Tanzania kuzikutanisha nchi 48 za Asia na Afrika

Muktasari:

  • Shirika la Mashauriano ya kisheria kwa nchi za Asia na Afrika (AALCO) lilianzishwa mwaka 1956 ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kufanyika kwa mkutano wa Bandung Indonesia 1955 uliozaa nchi zisizofungamana na upande wowote.

Dar es Salaam. Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa mashauriano ya kisheria kwa nchi za Asia na Afrika  (Asia, Afrika Legal Consultative Consultative Organization- AALCO) utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 21 hadi 25, 2019.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Oktoba 19, 2019 Dar es Salaam, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Augustine Mahiga amesema kufanyika kwa mkutano huo nchini ni nafasi ya Tanzania kuonyesha mapinduzi ya kisheria yaliyofanywa na Rais wa nchi hiyo, John Magufuli likiwamo suala la kusamehe wahujumu uchumi.

“Kufanyika kwa mkutano huu ambazo kuna mapinduzi yaliyofanywa na Rais John Magufuli ya kisheria, commitment (kujitoa kwake) yake na mapambano dhidi ya rushwa imebidi zitungwe sheria. Wenzetu tutawaeleza tunafanya nini,” amesema Dk Mahiga.

Amesema mkutano huo utakaofunguliwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya Rais Magufuli utahudhuriwa na mawaziri wa sheria kutoka nchi 48 za Asia na Africa.

Alitaja mambo yatakayojadiliwa kuwa pamoja na sheria ya kimataifa ya bahari, kuvunjwa kwa sheria ya kimataifa nchini Palestina na maeneo mengine yanayoshikiliwa na chi ya Israel na masuala mengine yanayohusiana na Palestina.

Mengine ni pamoja na sheria ya kimataifa katika masuala ya mitandao, utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani, sheria ya kimataifa katika suala ya biashara na uwekezaji, matumizi ya sheria za nje ya nchi, vikwazo dhidi ya nchi nyingine na Tume ya sheria ya kimataifa.

Alisema shirika hilo lilianzishwa mwaka 1956 wakati nchi nyingi za Asia na Afrika zikiwa bado kwenye ukoloni.

“Lengo lilikuwa ni kuendeleza ukombozi wa nchi ambazo bado zilikiwa hazijakombolewa. Chombo hiki kiliundwa ili kutumika kama jukwaa la ushauri wa wataalamu katika kubadilishana taarifa na maoni kwa nchi za Asia na Afrika,” amesema

Ametaja nchi zilizoanzisha ni pamoja na Burma (kwa sasa Myanmar), Ceylon (kwa sasa Sri Lanka), India, Iraq, Japan, Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu, Misri na Syria.

Amesema Tanzania ilianza kushiriki mikutano ya AALCO mwaka 1965 lakini ilikuja kujiunga rasmi mwaka 1973.

Akifafanua zaidi kuhusu shirika hilo, Katibu Mkuu  wa AALCO, Profesa Kennedy Gaston amesema lina lengo la kujadili masuala ya sheria kabla ya kwenda Umoja wa Mataifa, kutoa ushauri kuhusu sheria za kimataifa, kujange uwezo kwa sheria na maeneo mapya ya sheria za kimataifa na kuendeleza sheria za kimataifa hasa biashara na uwekezaji.