Serikali ya Tanzania mbioni kuanza mradi kutambua mmiliki wa ardhi

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Ardhi Nicholas Mkapa akikagua baadhi ya vifaa vinavyotumika kukagua ardhi wakati wa kongamano la wapima ardhi jijini Dar es Salaam

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana Benki ya Dunia (WB) itatekeleza mradi wa kupima na kutambua mmiliki wa ardhi nchini.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana Benki ya Dunia (WB) itatekeleza mradi wa kupima na kutambua mmiliki wa ardhi nchini.

Upimaji huo unaelezwa kuwa utasaidia kumaliza migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali kwa sababu wamiliki wa maeneo hayo watatambuliwa.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Novemba 14, 2019 na katibu mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nicholas Mkapa wakati akifungua kongamano la Wapima Ardhi Tanzania (IST).

Amesema mradi huo unatarajiwa kutekelezwa na wapima ardhi wa ndani ya nchi  ili kutoa ajira na kuwajengea uwezo.

Amesema wizara hiyo imekamilisha kazi ya kuunda mfumo mpya wa upimaji wa ardhi utakaotumika kutekeleza kazi zote za upimaji.

“Mfumo huu unaendana na mfumo unaotumika kimataifa ambao unatumia taarifa zilizoboreshwa kuhusu ukubwa na umbo la dunia.”

“Mfumo huu umekamilika na upo tayari kutumika,  na utatangazwa kwenye gazeti la Serikali mwisho mwa 2019 au mapema mwaka 2020,” amesema Mkapa.

Amesema kwa sasa Serikali imeunda kanda nane za ardhi ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

“Siku hizi kazi zote za upimaji, mipango miji na utoaji wa hati zinafanyika kwenye kanda na hii imeondoa usumbufu kwa sababu hazilazimishi mtu asafiri kuja Dar es Salaam,” amesema.

Awali Rais wa Wapima Ardhi, Bille Mussa aliiomba wizara hiyo kuendeleza ushirikiano uliopo baina yao ili kuondoa migongano kati ya wataalamu na  kupunguza migogoro ya ardhi inayoathiri wananchi.