Tanzania yaanza kusambaza vitabu shuleni

Muktasari:

  • Ili kuendana na sera ya elimu kuhusu uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), imeanza kusambaza vitabu hivyo.

Dar es Salaam. Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imetumia Sh12.9 bilioni kuandika na kuchapa vitabu vya shule za awali, msingi na sekondari ili kumaliza uhaba wa vifaa hivyo shuleni.

Vitabu hivyo vimeanza kusambazwa jana Ijumaa Januari 17,2020 kwa ushirikiano baina ya taasisi hiyo na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) huku mkoa wa Ruvuma ukiwa wa kwanza kupelekewa.

Akizindua usambazaji huo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo alizitaka halmashauri kutofungia vitabu makabatini badala yake wafikishe shuleni.

“Kumekuwa na kasumba ya ucheleweshaji wa vitabu hivi, halmashauri fikisheni vitabu hivi mapema msikae navyo tena,” alisema.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TET, Dk Aneth Komba alisema wakati JKT wakitoa magari na maofisa wa kusaidia usambazaji huo, ofisi yake imechangia mafuta.

“Tunachofanya vitabu hivi tutavipeleka mpaka halmashauri, kisha halmashauri zitasambaza shuleni,” alisema.

Alisema vitabu hivyo vitamaliza uhaba  shuleni na kwamba, kwa sasa wamefikia hatua ya wanafunzi watatu kusoma kitabu kimoja.

“Kwa shule binafsi vitabu vinapatikana kwa bei nafuu kurudisha gharama kidogo. Vitabu hivi vimechapwa kwa fedha za mapato ya ndani,” alisema,