Tanzania yafanikiwa viwango utokomezaji Ukoma

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiwa katika kijiji cha msamalia wanapoishi watu walioathirika na ugonjwa wa Ukoma kilichopo Hombolo mkoani Dodoma

Muktasari:

Wakati dunia ikiadhimisha siku ya ugonjwa wa ukoma leo Januari 26, nchi ya Tanzania viwango vya utokomezaji vimeendelea kuboreshwa na kushusha idadi ya waathirika wa ukoma kutoka wagonjwa 4.3 kati ya watu 100,000 mnamo mwaka 2014 na kufikia wagonjwa 3 kati ya watu100,000 mwaka 2019

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema Tanzania tayari imefikia viwango vya kidunia vya utokomezaji wa ugonjwa huo vya kuwa na chini ya wagonjwa 10 kati ya watu 100,000.

Waziri Ummy ameyasema hayo jana Jumamosi Januari 26, 2020 wakati akitoa tamko la siku ya Ukoma duniani kwenye makazi ya waathirika wa ugonjwa huo yaliyopo kijiji cha msamalia kilichopo Hombolo mkoani Dodoma. Siku ya ukoma dunia huadhimishwa Januari 26, 2020.

“Kutokana na juhudi za Serikali, viwango hivyo vya utokomezaji vimeendelea kuboreshwa na kushusha idadi ya waathirika wa ukoma kutoka wagonjwa 4.3 kati ya watu 100,000 mnamo mwaka 2014 na kufikia wagonjwa watatu kati ya watu100,000 mwaka 2019."

Amesema jitihada kubwa za Serikali zimeweza kupunguza viwango vya maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukoma kutoka wagonjwa 43 kati ya watu milioni moja mwaka 2014 hadi kufikia wagonjwa 26 kwa watu milioni moja mwaka 2019.

"Vile vile, tumepunguza idadi ya watoto wanaougua ukoma kwa asilimia 41, kutoka watoto 90 mwaka 2014, hadi 53 mwaka 2019. 

Hata hivyo Waziri Ummy amesema hadi kufikia mwaka 2019, mikoa yote isipokuwa Lindi ilikuwa tayari imefikia kiwango cha utokomezaji.

Waziri huyo amesema zipo Halmashauri 16  ambazo bado hazijafikia viwango hivyo na kuzitaja  Halmashauri hizo ni pamoja na Manispaa ya Lindi, Liwale, Nachingwea, Ruangwa, Masasi, Nanyumbu, Morogoro, Mvomero, Mpanda, Nkasi, Manispaa ya Shinyanga, Manispaa ya Kigoma, Kibaha, Mkinga na Tunduru.

“Nipende kuzikumbusha Halmashauri hizi na mikoa kuongeza kasi ya kutokomeza Ukoma na kuhakikisha kaya zote hatarishi na zenye wagonjwa wa Ukoma zinafikiwa, wanakaya wanachunguzwa dhidi ya ugonjwa wa Ukoma na wale ambao tayari wanaugua wanatibiwa kikamilifu," amesisitiza Waziri Ummy

Waziri Ummy aliitaka Mikoa na Halmashauri zihakikishe zinatenga bajeti katika mipango yao ili kuendesha kampeni za uhamasishaji, uelimishaji, na uibuaji wa wagonjwa wapya, kauli mbiu ya siku ya Ukoma duniani mwaka huu ni"Tuthamini haki na utu wa waathirika wa ukoma kwa kutokomeza ubaguzi, unyanyapaa na chuki."