Tanzania yajiimarisha kukabiliana na maafa

Muktasari:

Waziri Mhagama amesema lengo la serikali ya Tanzania kutunga Sheria ya Usimamizi wa Maafa ya kitaifa Na. 7 ya 2015 ni moja ya hatua ya uimarishaji wa uwezo wa usimamizi wa Maafa yatakayotokea nchini

Unguja. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama amesema katika uimarishaji uwezo wa usimamizi wa maafa Serikali ya Tanzania imetunga Sheria ya Usimamizi wa Maafa ya kitaifa Na. 7 ya 2015 pamoja na kanuni zake ambayo itakuwa msingi mkubwa wa kukabiliana na majanga ya maafa.

Mhagama ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Februari 21, 2020 katika uzinduzi wa mkutano wa kwanza wa kamati ya mawaziri wenye dhamana ya masuala ya kukabiliana na maafa  wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika hoteli ya Madinat-Bahar Mbweni mjini Unguja.

Amesema lengo kubwa la Serikali ni kuhakikisha kila sekta inazingatia hatua za upunguzaji madhara ya maafa katika mipango ya maendeleo na uandaaji bajeti ili kupunguza madhara kwa jamii na hasara za uchumi.

Mhagama amesema licha ya juhudi hizo, kupitia mkutano huo wa kwanza wa kamati ya mawaziri wanaohusika na menejimenti ya maafa kwa nchi wanachama wa SADC, unakusudia kuchochea juhudi zilizopo kupunguza madhara ya maafa.

“Lakini mkutano wetu huu tutajadili na kupitisha mkakati wa kujiandaa na kukabiliana na maafa wa kikanda kwa mwaka 2016 – 2030, pamoja na kujadili na kuridhia mfumo mkakati wa ustahimilivu wa kikanda kwa mwaka 2020-2025,” amesema.