Tanzania yapendekeza Kiswahili kupandishwa hadhi Umoja wa Mataifa

Tuesday October 22 2019

By Gadi Solomon, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN), Balozi Modest Mero ametoa wito Kiswahili kuwa lugha rasmi ya saba katika umoja huo.

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika kikao cha wajumbe wa kamati ya nne ya umoja huo jana Jumatatu, Oktoba 21, 2019.

“Tayari Kiswahili ni lugha rasmi katika Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Bunge la Afrika Mashariki na hivi karibuni ilitangazwa kuwa lugha rasmi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),” amesema.

Katika mkutano huo uliofanyika Marekani, Balozi Mero amesema lugha hiyo hivi sasa inatumika katika vyombo vingi vya habari vya kimataifa.

Amesema ipo haja ya nchi zinazotumia lugha hiyo kuwekwa katika orodha ili kuimarisha ushiriki wa nchi husika katika umoja huo.

“Hii itawezesha kitengo hicho kufanya kazi yake kwa ufanisi kwa ajili ya wazungumzaji wa Kiswahili kupitia televisheni, redio na mitandao ya kijamii,” amesema  Balozi Mero.

Advertisement

Balozi huyo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha kitengo cha habari kwa kuwaajiri wataalamu wa Kiswahili vijana kutoka nchi zinazozungumza lugha hiyo ili kuongeza ufanisi.

Ikiwa Kiswahili kitapitishwa kitaongeza idadi ya lugha za umoja huo kuwa saba baada ya Kifaransa, Kiingereza, Kihispania, Kichina, Kirusi na Kiarabu.

Akizungumzia pendekezo hilo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Dk Selemani Sewangi amesema hiyo ni hatua nzuri kukipeleka Kiswahili kwenye umoja huo.

 “Juhudi za kukitangaza Kiswahili kimataifa zinaonekana, pia turudi hapa nchini kwa kukipa majukumu ili kitumike katika mawanda mapana,” amesema Dk Sewangi.

Advertisement