Tanzania yapewa Sh240 bilioni kuboresha sekta ya elimu

Muktasari:

  • Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE) umeipatia Serikali ya Tanzania Sh240.95 bilioni kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu.

Dar es Salaam. Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE) umeipatia Serikali ya Tanzania Sh240.95 bilioni kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu.

Kati ya fedha hizo,  Sh88.55 bilioni zitatumika katika mpango wa maendeleo ya sekta ya elimu na Sh116.40 bilioni kwa ajili ya nyongeza ya mchango wa Sweden katika Programu ya Elimu kwa Matokeo (EPforR).

Akizungumza leo Jumatano Januari 15, 2020 katika hafla ya kusaini mikataba miwili ya msaada kati ya Tanzania na Sweden, katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango wa Tanzania, Doto James amesema msaada huo ni muhimu kwa sababu utaongeza ufanisi katika sekta ya elimu.

"Naushukuru mfuko wa ushirikiano wa elimu duniani na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Sweden(Soda) kama wakala wa mfuko kwa msaada huu mkubwa," amesema James.

Katibu mkuu wa Wizara ya Elimu, Dk Leonard Akwilapo amesema msaada huo utaimarisha ufundishaji hasa elimu ya msingi.

Ameahidi fedha hizo zitatumika kama zilivyopangwa, zitasaidia kuboresha miundombinu iliyolemewa na idadi kubwa ya wanafunzi kutokana na elimu bila malipo.

"Makubaliano haya yamesubiriwa muda mrefu, tunashukuru kwa msaada huu utakaoboresha mazingira ya elimu kwa matokeo bora," amesema.

Awali, balozi wa Sweden nchini Tanzania, Anders Sjoberg aliipongeza Serikali kwa kufanikisha elimu bila malipo na kuahidi ushirikiano katika kuboresha sekta ya elimu.