Tanzania yashauriwa kutumia teknolojia ya datawazi

Muktasari:

Miongoni mwa changamoto ambazo Serikali ya awamu ya tano iliamua kuanza nazo ni kuwaondoa wafanyakazi hewa na wenye vyeti bandia suala ambalo kampuni kubwa ya utengenezaji wa nyaraka duniani, Société Industrielle et Commerciale de Produits Alimentaires (Sicpa) inasema inaweza kumalizwa kwa teknolojia hii mpya.

Dar es Salaam. Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani inaweza kudhibiti nyaraka na takwimu zake muhimu kwa kutumia teknolojia ya datawazi (blochachain), wataalamu wameshauri.

Licha ya maeneo hayo, teknolojia hiyo pia inaweza kudhibiti bidhaa bandia sokoni kwa kuwapa wateja uwezo wa kuthibitisha mtengenezaji pamoja na kuboresha utendaji kazi za kitaaluma kama uhasibu, rasilimaliwatu na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Miongoni mwa changamoto ambazo Serikali ya awamu ya tano iliamua kuanza nazo ni kuwaondoa wafanyakazi hewa na wenye vyeti bandia suala ambalo kampuni kubwa ya utengenezaji wa nyaraka duniani, Société Industrielle et Commerciale de Produits Alimentaires (Sicpa) inasema inaweza kumalizwa kwa teknolojia hii mpya.

“Blockchain (datawazi) zinahakikisha hatua zote zinafuatwa na kuzingatiwa kwenye nyaraka na taarifa muhimu za Serikali. Inapunguza gharama, inaondoa uwezekano wa kughushi bila kujulikana na uandaaji wa takwimu zisizo sahihi. Inaongeza kuaminika kwa Serikali mbele ya wananchi,” inasema kampuni hiyo.

Ushauri huo umetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye kongamano la mapinduzi ya nne ya viwanda lililoandaliwa na Sahara Sparks na kufanyika jijini hapa likiwakaribisha watalamu wa teknolojia kutoka kila pembe ya dunia.

Wakiwasilisha mada kwenye kongamano hilo, wataalamu wa kampuni ya Sicpa, Marco Aloe na Philippe Thévoz walisema wanaitumia teknolojia ya datawazi kudhibiti ubora wa kila bidhaa wanayoitoa jambo linaloweza kufanywa na Serikali ya Tanzania hata kampuni binafsi zilizopo nchini pamoja na mashirika ya umma.

Kampuni hiyo yenye matawi kwenye mataifa 35 duniani ikihudumia wateja waliopo katika nchi 160 kutoa huduma za udhibiti na ufuatiliaji wa nyaraka, uwekaji wa alama za siri kwenye noti za nchi mbalimbali na ulinzi wa nembo za bidhaa kwa zaidi ya miaka 90 sasa, inasema teknolojia ya datawazi ni mapinduzi yanapaswa kuhimizwa kwa kila mtu.

“Iwe cha kuzaliwa, usajili wa biashara au leseni ya udereva, cheti kilichotengenezwa kwa teknolojia hii hakiwezi kughushiwa kwa namna yoyote ile,” wanasema wataalamu hao.

Datawazi ni jukwaa linaloruhusu shughuli za aina tofauti kulingana na mahitaji ya mtumiaji. Tayari inatumika katika utengenezaji wa sarafu za kidijiti ikiwamo maarufu ya bitcoin.

Maeneo mengine ambako Sicpa wanatumia teknolojia ya datawazi ni utoaji wa hati za ardhi, vitabulisho vya kidijiti, usajili wa kodi na huduma za afya. Tangu mwaka 2008, Estonia imekuwa ikitumia teknolojia hiyo pia kutoa huduma zake zote kwa wananchi.

Mkurugenzi wa kampuni ya Veridoc Global iliyoshiriki kongamano hilo pia, Alex Mhagama alisema Serikali ipo katika mabadiliko ya maendeleo kuelekea uchumi wa kati yaayohitaji matumizi ya teknolojia ya uhakika.

Kufanikisha vipaumbele kama kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato, kuwezesha miamala ya kidigiti na kuunganisha mifumo ya Tehema ya taasisi zote za Serikali na wadau wengine wa biashara ni sual alinalotekelezeka kwa urahisi zaidi ukitumia teknolojia ya datawazi,” alisema Mhagama.

Veridoc inatoa huduma zinazotumia teknolojia hiyo ambayo Mhagama alisema ina uhakika wa kuimarisha usalama wa raia na Taifa, kulinda maliasili za nchi na kuboresha miundombinu ya usafiri.