Tanzania yatajwa kuwa na utalii mkubwa wa mawasiliano

Wednesday September 18 2019

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema nchi ina utalii mkubwa wa mawasiliano unaoweza kuleta mapinduzi makubwa ya maendeleo katika sekta nyingine kwa nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).

Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari leo Jumatano Septemba 18, 2019 Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Uchukuzi, Habari, Hali ya Hewa na Mawasiliano Dk Jim Yonazi amesema nchi imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika sekta ya mawasiliano.

Dk Yonazi ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya Mawasiliano) amesema Tanzania inafanya vizuri katika sekta ya mawasiliano na miundombinu ya sekta hiyo ikiwamo kufikia viwango vya 4G na kusambazwa kwa Mkongo wa Taifa nchi nzima.

“Katika sekta ya mawasiliano hatuna wasiwasi. Tuko vizuri kwa maana ya miundombinu na wananchi wengi wamefikiwa na huduma ya mawasiliano yakiwamo ya simu na intaneti. Wenzetu wa nchi za Sadc tunawakaribisha si tu katika mikutano hii ya kisekta, bali waje kujifunza utalii mkubwa wa mawasiliano,” amesema Dk Yonazi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), mpaka Desemba mwaka 2017, Tanzania ilikuwa na watumiaji wa intaneti zaidi ya milioni 23, sawa na asilimia 45 ya idadi ya Watanzania wote.

Kati ya watumiaji hao, 83 kwa kila 100 wanatumia intaneti inayohamishika (mobile wireless) inayotumia zaidi simu za mkononi, tableti na kompyuta mpakato (laptop). Na watumiaji wawili kwa kila 100 hutumia intaneti ya waya isiyohamishika (fixed wired).

Advertisement

Advertisement