Tanzania yawakaribisha wawekezaji 80 kutoka China

Washiriki wa Kongamano la kibiashara kati ya Tanzania na China linalofanyika jijini Dar es Salaam leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema hivi sasa ipo katika mkakati wa kujikomboa kiuchumi baada ya kupata uhuru wa kisiasa, kuiomba nchi ya China kuiunga mkono.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema hivi sasa ipo katika mkakati wa kujikomboa kiuchumi baada ya kupata uhuru wa kisiasa, kuiomba nchi ya China kuiunga mkono.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Septemba 5, 2019 na mkurugenzi wa Mamlaka Ukanda wa Uwekezaji Tanzania (EPZA), Joseph Simbakalia alipokuwa akiukaribisha ujumbe wa wafanyabiashara na wawekezaji 80 kutoka China waliotembelea viwanda vilivyopo chini ya mamlaka hiyo.

"Sasa hivi tupo kwenye awamu ya pili ya ukombozi, tunautafuta uhuru wa kiuchumi. China ni rafiki yetu wa muda mrefu, tunawakaribisha mje kuwekeza hapa na kunufaika na soko kubwa la Afrika Mashariki (EAC) na SADC," amesema Simbakalia.

Simbakalia amewahakikishia wageni hao mazingira bora na rafiki ya uwekezaji na ufanyaji biashara.

Licha ya kutembelea EPZA, wageni hao wametembelea pia soko la Kimataifa Kariakoo, reli ya Tazara pamoja na ofisi za ubalozi wa China nchini kisha kushiriki kongamano la kibiashara baina yao viongozi wa Serikali, sekta binafsi nchini pamoja na Wachina waliowekeza Tanzania.

Simbakali amemshukuru mratibu wa kongamano hilo, kampuni ya Linghang Group na kuahidi kuendelea kuipa ushirikiano unaohitajika i kuendelea kuwaalika wawekezaji wengi zaidi.

Meneja wa Linghang Group, Cathy Wang amesema wataendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine muhimu kufanikisha uwekezaji nchini.