Tasaf watumia Sh1.4 trilioni kunusuru kaya masikini

Muktasari:

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf) umetumia Sh1.46 trilioni kutekeleza miradi ya kunusuru kaya masikini katika  kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu ya mfuko huo.

Dar es Salaam. Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf) umetumia Sh1.46 trilioni kutekeleza miradi ya kunusuru kaya masikini katika  kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu ya mfuko huo.

Fedha hizo zimetumika katika kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu ya mfuko huo kilichoanza kutekelezwa mwaka 2013 na kukamilika Desemba, 2019.

Mfuko wa Tasaf ulianzishwa mwaka 2000 kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo lengo likiwa ni kupunguza umaskini kwa kutumia dhana ya ushirikishwaji jamii.

Mkurugenzi mtendaji wa Tasaf, Ladslaus Mwamanga amesema zaidi ya kaya milioni 1.1 zenye watu milioni 5.2 ziliandikishwa kwenye mpango na kupata ruzuku stahiki.

Akizungumza katika uzinduzi wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya Tasaf jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Februari 17, 2020, Mwamanga amesema utekelezaji wa kunusuru kaya masikini umefanyika katika mamlaka za Serikali za mitaa 159 Tanzania Bara huku Zanzibar ukifanyika kwenye wilaya zote.

Ametaja maeneo yaliyofanyiwa kazi ni kunusuru kaya masikini, ajira za muda kwa kaya masikini na kuongeza kipato kwa kaya masikini kupitia uwekaji akiba na kujiimarisha kiuchumi.

Maeneo mengine ni  kujenga na kuboresha miundombinu ya sekta za elimu, afya na maji.

Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mfuko huo kati ya mwaka 2000 mpaka 2005, miradi 1,704 ya Sh72 bilioni ilitekelezwa.

Ameeleza kuwa katika awamu ya pili ya Tasaf iliyoanza mwaka 2005 mpaka 2013, miradi zaidi ya 12,000 ya Sh430 bilioni ilitekelezwa.

“Awamu ya tatu ya Tasaf ndiyo inayotekelezwa sasa na utekelezaji wake ulianza mwaka 2013 ukitarajiwa kuisha mwaka 2023,” amesema mkurugenzi huyo.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.