USHAURI WA DAKTARI: Testosterone, kichochezi nyeti kwa wanaume kikipungua sauti huwa nyembamba na kupoteza mwonekano wa kiume

Kichochezi cha Testosterone ndicho kichochezi nyeti kwa mwanaume kutungisha mimba, kuwa na misuli mikakamavu, mtawanyiko wa mafuta mwilini na utengenezwaji wa chembe hai nyekundu.

Inapotokea kiwango cha kichochezi hiki kuwa chini kuliko kawaida mwanaume hupata matatizo kama kusinyaa maumbile ya kiume na ugumba. Kuendelea kwa maendeleo ya kisayansi kwenye uchunguzi miaka ya sasa imewezesha kugundulika upungufu wa kichochezi hiki kwa baadhi ya wanaume.

Tatizo hili limechangia uwepo wa uhitaji virutubisho maalum vya kuchochea utengenezwaji wa kichochezi hiki mwilini mara tano zaidi kuliko miaka kumi iliyopita. Kwa kawaida kokwa za kiume hutengeneza vichochezi vya kiume vinavyojulikana kama Androgens ambayo kazi zake ni kuchochea ukuaji wa mfumo wa viungo vya uzazi, misuli imara, sauti nzito na bezi vile vile kupata ashiki ya kujamiiana.

Kichochezi cha Testosterone ni moja ya aina muhimu ya Androgen inayojulikana zaidi. Kwa kawaida kokwa zenye afya huweza kutengeneza kwa siku miligramu 6 za kichocheo hicho.

Pia kokwa za kiume hutengeneza karibu wastani wa mbegu za kiume 200,000 kwa dakika, ingawa kadri umri wa mwanaume unavyosonga (miaka zaidi ya 30 ) kiwango cha uzalishaji hupungua.

Ukiacha athari inayosababishwa na umri, yapo matatizo ya kiafya ambayo yanasababishwa au kuchangia kupungua kwa kiwango cha Testosterone.

Kwa kawaida mwanaume aliyezaliwa bila hitilafu ya kimaumbile huwa na kokwa mbili (testicle) au hujulikana pia kama kende, huundwa ndani ya tumbo kabla ya kuzaliwa na hapo baadaye hushuka wakati mimba ikiwa na miezi saba. Katika hatua hii baadhi ya watoto huzaliwa na hitilafu ya kende kutoshuka katika pochi ya kuhifadhia kokwa.

Tatizo hili huwapata asilimia mbili ya watoto wa kiume wanaozaliwa huku asilimia 10 ya wanaozaliwa kokwa zote mbili zikiwa zimekaa vibaya.

Matatizo ya kiafya yanayosababisha upungufu wa Testosterone ni pamoja na lishe duni, kutopumzika au kutokulala saa za kutosha, magonjwa sugu na ajali za maeneo ya uzazi. Pia magonjwa ya kurithi, uvimbe katika tezi zilizopo katika ubongo, kujeruhiwa katika kokwa, ulevi au matumizi ya dawa za kulevya na sumu au kemikali zilizoingia mwilini.

Dalili za upungufu wa homoni hii ni pamoja na ugumba, upungufu wa nguvu za kiume, tishu za maziwa kuvimba, kukosa hamu ya kujamiiana, nywele za mwilini kupungua, sauti kuwa nyembamba, misuli kupungua uimara, uume na nyumba ya kokwa kuwa ndogo.

Kwa kawaida vijana wa kiume huanza kuingia balehe kuanzia miaka 10, hatua hii ikichelewa upo uwezekano wa kijana huyo na upungufu wa Testosterone.

Kwa kawaida kichochezi hiki hufikia kiwango cha juu mwanaume anapokuwa amefikisha umri wa kati ya miaka 20-30, baada ya miaka 30-40 inakadiriwa kushuka kwa asilimia moja.

Kichochezi hiki kipo kwa kiasi kidogo kwa wanawake, na pale kinapozidi kwa kiwango kikubwa husababishwa mwanamke kuwa na sauti nzito, kutoka vinyweleo, kuwa na misuli mikakamavu na hata ugumba. Kichochezi hiki kwa mwanaume ndio msingi wa mwanaume kuwa na hamu ya kujamiiana, uwezo wa kutungisha mimba na kupata maumbile yanayomtambulisha kuwa ni mwanaume, hivyo mwanaume akiona ana viashiria au dalili nilizoeleza vizuri afike katika huduma za afya kwa ushauri.