Tisa waunganishwa kesi ya kina Halima Mdee

Muktasari:

Watu tisa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuunganishwa katika kesi ya viongozi na wafuasi 15  wa Chadema wanaokabiliwa mashitaka saba likiwemo la kukaidi amri halali, kutoa lugha ya maudhi na kuharibu geti la gereza la Segerea.

Dar es Salaam. Watu tisa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuunganishwa katika kesi ya viongozi na wafuasi 15  wa Chadema wanaokabiliwa mashitaka saba likiwemo la kukaidi amri halali, kutoa lugha ya maudhi na kuharibu geti la gereza la Segerea.

Washtakiwa hao ni Ahumani Hassan, Omary Milodo, Emmanuel Ignastemu, Stephen Kitomali, Hamis Yusuph, Juma Juma, Mustafa Lada, Emmanuel Zakaria na Steven Ezekiel

Awali washtakiwa 15 walifikishwa mahakamani hapo Machi 23, 2020 wakiwemo wabunge watatu wa chama; Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda) na Jesca Kishoa (Viti maalumu).

Washitakiwa wengine  ni  Meya wa manispaa ya Ubungo,  Boniface Jacob; Diwani wa Tabata, Patrick Assenga;  Mshewa Karua, Khadija Mwago, Pendo Mwasomola, Cesilia Michael, Happy Abdallah, Stephen Kitomali na Paulo Makali.

Akisoma hati ya mashtaka leo Alhamisi Aprili 2, 2020 wakili wa Serikali, Ester Martine amedai Machi 13, 2020 washtakiwa wote  wakiwa katika gereza la Segerea lililopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam isivyo halali kwa makusudi walikaidi amri iliyotolewa na askari B 3648 SGT John ambaye  aliwataka wahusika hao kuondoka eneo hilo la magereza na alikuwa akitimiza wajibu wake aliyopewa.

Katika shtaka la pili la kufanya mkusanyiko usio halali, Inadaiwa Machi 13, 2020 katika eneo la gereza la Segerea lililopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, washitakiwa kwa pamoja walikusanyika katika eneo hilo isivyo halali hali iliyopelekea kuleta hofu na kuhatarisha amani na utulivu kwenye eneo hilo.

Shtaka la tatu la kuharibu mali, inadaiwa  kuwa Machi 13,2020 eneo la gereza la Segerea lililopo Wilaya ya Ilala washtakiwa walishirikiana kufanya uharibifu wa geti la Segerea ambalo ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika shitaka la nne la kutoa lugha ya kuudhi ambalo linamkabili Mdee, Inadaiwa Machi 13, 2020 katika gereza la Segerea mshitakiwa alitoa maneno ya kuudhi kwa askari magereza Sajenti B 3648 John, maneno ambayo yalipelekea uvunjifu wa amani.

Shtaka la tano ambalo nalo ni la kutoa lugha ya kuudhi linamkabili Bulaya anayedaiwa Machi 13, 2020 akiwa maeneo ya gereza la Segerea alitoa maneno ya kuudhi kwa Sajenti B 3648 John na kupelekwa uvunjifu wa amani.

Shtaka la sita linalomkabili Jacob, inadaiwa alitamka maneno ya kuudhi kwa Sajenti huyo.

Katika shitaka la mwisho, inadaiwa kuwa Machi 13, 2020 Jacob alifanya shambulio kwa askari magereza kwa kumkunja na kumvuta shati wakati akitekeleza majukumu yake.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana kutenda makosa hayo, upande wa Jamhuri umedai  upelelezi wa shauri hilo umekamilika hivyo wanaomba tarehe kwa ajili ya kuja kuwasomea maelezo ya awali.

Hakimu Mwandamizi, Vicky Mwaikambo amesema kila mshtakiwa anatakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bodi ya Sh400, 000 na kuwa na barua inayotambulika nne.

Washtakiwa wawili kati ya tisa waliofikishwa mahakamani hapo wametimiza masharti ya dhamana.