Top 5, magari ya bei ghali kwa sasa

Wednesday August 14 2019

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mambo mengine ukiyasikia utadhani ni masihara hasa ukwasi wako unapokuwa dhoofu, fikiria jumla ya thamani ya mali zako haifikii hata Sh5 milioni na akaunti yako ya fedha benki inasoma chini ya tarakimu 5 halafu unasikia mtu amenunua gari aina ya Bugatti La Voiture Noire.

Bugatti la voiture noire, inatajwa kuwa ndiyo gari ya gharama kubwa kuliko gari zote duniani, ikiuzwa kwa Dola 19 milioni za Marekani sawa na Sh43.7 bilioni.

Gharama ya Bugatti la voiture noire moja ni sawa na kununua gari aina ya Toyota IST 4,375 za milioni kumi na ni kubwa kuliko bajeti ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo ya mwaka huu, ambayo ni Sh30 bilioni ikiwa ni pungufu kidogo ya bajeti ya Wizara ya Madini ambayo ni Sh49 bilioni.

Gari hiyo inayotengenezwa nchini Ufaransa, ina uwezo wa kufikia spidi 300 ndani ya sekunde 13.3 na ina uwezo wa kukimbia kilometa 465 kwa saa (Spidi).

Ukiachilia mbali Bugatti la voiture noire, gari ya pili kwa kuuzwa fedha ndefu ni Rolls-Royce Sweptail inayotengenezwa Uingereza  ambayo inauzwa Dola 13 milioni Marekani sawa na Sh29.9 bilioni.

Namba tatu ni Mercedes-benz may Bach Exelero, inayotengenezwa nchini Ujerumani, gharama yake ni Dola 8 milioni  za Marekani sawa na Sh18.4 bilioni.

Advertisement

Namba nne ni gari aina ya Koenigsegg Ccxr Trevita inayotengenezwa nchini Swiden inayouzwa dola milioni 4.8 sawa na Sh11 bilioni.

Na katika orodha, namba tano inashikiliwa na gari aina ya Lamborghini Veneno inayouzwa Dola 4.5 milioni, sawa na Sh10.3 bilioni.

Advertisement