Treni Dar es Salaam - Moshi yaanza safari leo na mabehewa manane

Muktasari:

Treni  ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi kwa mara ya mwisho ilifanya safari kati ya Dar es Salaam na Moshi  mwaka 1994.


Dar es Salaam. Leo Ijumaa Desemba 6, 2019 Saa 10:00 jioni, treni  ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi imeanza kutoa huduma ya usafiri baada ya kupita miaka 25.

Mara ya mwisho treni hiyo kufanya safari kati ya Dar es Salaam na Moshi  ilikuwa mwaka 1994.

Ikiwa na mabehewa manane ya daraja la pili kulala na kukaa pamoja na daraja la tatu imeondoka jijini Dar es Salaam na abiria zaidi ya 700.

Wakati abiria wanaosafiri kutoka Dar es Salaam hadi Moshi mkoani Kilimanjaro, nchini Tanzania wakitumia saa kumi hadi 11 njiani kufika kwa usafiri wa basi, katika treni itawalazimu kutumia saa 16.

Safari za treni hiyo kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi itakuwa ni siku za Jumanne na Ijumaa Saa 10 jioni na kuwasili Moshi Saa 2 asubuhi, kutoka Moshi kwenda Dar es Salaam itakuwa ni Jumatano na Jumamosi Saa 10 jioni na kuwasili Dar es Salaam Saa 2 asubuhi.

Mkuu wa kitengo cha habari na uhusiano wa TRC, Jamila Mbarouk amesema, “muda njiani ni mrefu kwa kuwa ndio tunaanza ikizingatiwa njia haijatumika muda mrefu. Hatuwezi kuanza kutembea mwendo mkali. Baadaye muda wa kukaa njiani utapungua.”

“Watu wamejitokeza wengi na hadi inaondoka tunatarajia kuwa na abiria zaidi ya 700.”

Umbali kutoka Dar es Salaam hadi Moshi ni kilomita 558, treni hiyo itapita vituo 12 ambayo ni Wami, Mkalamo, Gendagenda, Mnyusi, Korogwe, Mombo, Mkomazi, Hedaru, Makanya, Same, Kisangiro na Kahe ambacho ni kituo cha mwisho kabla ya kuingia Moshi.

Mmoja wa abiria, Swedy Machenje amesema, “ni usafiri mzuri licha ya kutumia muda zaidi ya basi. Nimependa nauli ni ndogo na pia sijawahi kupanda treni. Ni  mara yangu ya kwanza naamini treni hii itakuwa msaada sana.”

Abiria mwingine, Joanitha Jacob amesema, “mimi ni mfanyabiashara ilikuwa niondoke na basi ila baada ya kuona inaanza leo (treni) nikasema acha nikate tiketi nipate na muda wa kulala kabisa. Kesho nikifika nafanya shughuli zangu kisha jioni narudi nayo Dar es Salaam.”