VIDEO: Treni ya abiria Dar- Moshi yatumia saa 19 kufika Moshi

Muktasari:

Treni ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi iliyoanza safari jana saa 10 jioni imewasili mjini Moshi mkoani Kilimanjaro leo Desemba 7, 2019 saa 5:30 asubuhi.

Moshi. Treni ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania imewasili mjini Moshi leo Jumamosi Desemba 7, 2019 saa 5:30 asubuhi.

Treni hiyo iliyoanza kutoa huduma ya usafiri baada ya miaka 25 iliondoka Dar es Salaam jana Ijumaa Desemba 6, 2019 saa 10:00 jioni na ilitarajiwa kufika Moshi leo saa 2 asubuhi. Imetumia saa 19 kutoka Dar es Salaam hadi Moshi badala ya saa 16.

Mamia ya wananchi walifurika stesheni ya mjini Moshi kuipokea treni hiyo iliyokuwa na mabehewa manane na abiria takribani 700.

Akizungumza baada ya kuwasili kwa treni hiyo mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), Gilliard Ngewe amesema usafiri wa treni ni salama zaidi kuliko kupanda basi.

“Usafiri wa barabara kuna makosa mengi ya binadamu lakini treni ni tofauti kwa kuwa inafuata reli tu. Mimi nimekuja Moshi kwa ndege tangu jana lakini nilikuwa nikimfuatilia dereva wa treni hii.”

“Kama angekuwa na mwendo ambao si rafiki hakika angeshushwa njiani. Na nilitumia simu tu kufuatilia kwa hiyo utaona jinsi ilivyo salama kwamba unajua mwendo na kila kitu kupitia simu. Kimsingi amekuja vizuri,” amesema Ngewe.

Mwenyekiti wa Bosi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), Profesa John Kondoro amesema, “treni ni ya majaribio bado haijaanza rasmi kuna maeneo ambayo ni korofi. Tumetoa maelekezo maeneo hayo yafanyiwe kazi ili ikitoka Dar es Salaam saa 10 jioni ifike Moshi saa 2 asubuhi kama inavyotakiwa.”

Mmoja wa wananchi hao, Gothbert Lameck amesema, “Tumefika hapa stesheni saa 1  asubuhi kuisubiri. Binafsi nitapanda inayokwenda Dar es Salaam leo saa 10 jioni. Nadhani nitaachana na kupanda mabasi naona treni ni salama zaidi.”

“Nimepanda treni hii ya Moshi- Dar es Salaam miaka ya 1980, kwa kweli nimefurahi kuona imerejea tena. Ninaipongeza Serikali kwa kuirudisha na kimsingi itakuwa msaada sana hasa kibiashara,” amesema Daniel Rafael.

Treni hiyo inatarajia kurudi Dar es Salaam leo saa 10 jioni.