Breaking News

Trump azishutumu Facebook, Twitter

Friday October 16 2020

 

By AFP

Washington, United States. Rais wa Marekani, Donald Trump ameishutumu mitandao miwili ya kijamii, Facebook na Twitter, kwa kuzuia muunganisho na habari iliyoandikwa na tovuti ya gazeti la New York Post inayolenga kuanika mipango ya kifisadi ya mpinzani wake mkuu, Joe Biden na mtoto wake wa kiume nchini Ukraine.

Gazeti hilo lilisema limeipata kompyuta iliyotelekezwa na Hunter Biden ambayo inaonyesha shughuli za kibiashara za baba yake nchini Ukraine.

Mara kwa mara makamu huyo wa zamani wa rais -- mteule wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais utakaofanyika Novemba 3 -- amekanusha kuhusika katika biashara hizo.

"Barua pepe zinabainisha jinsi gani Hunter Biden alimtambulisha mfanyabiashara wa Ukraine kwa baba yake ambaye ni makamu wa rais," kichwa cha habari cha gazeti hilo kinasomeka.

Wakati timu ya kampeni ikisema Biden hajawahi kukutana na mfanyabiashara huyo, Facebook na Twitter ziliweka udhibiti katika muunganisho wa habari hiyo, zikisema kulikuwa na maswali kuhusu ukweli wa suala hilo.

"Hii ni sehemu ya mchakato wa taratibu zetu kupunguza usambazaji wa taarifa," alisema msemaji wa Facebook, Andy Stone.

Advertisement

Twitter ilisema inapunguza utoaji wa taarifa kutokana na maswali kuhusu "asili ya jambo" lililojumuishwa katika habari.

Lakini wanachama wa Republican walichukizwa na kitendo hicho wakisema kimefanywa kinazi.

Trump, ambaye anazidiwa na Biden katika kura za maoni ikiwa ni siku 20 kabla ya kupiga kura za rais, aliishambulia mitandao hiyo miwili ya kijamii.

"Ni kitu cha ajabu kwamba Facebook na Twitter hazijaichukulia kwa uzito habari ya barua pepe za 'Smoking Gun' zinazohusiana na Joe Biden na mtoto wake wa kiume, Hunter, katika akaunti ya @NYPost," alisema Trump katika akaunti yake ya Twitter.

"Huu ni mwanzo tu kwao. Hakuna kitu kibaya kama wanasiasa mafisadi."

Katika mkutano wa kampeni wa Iowa, Trump alisema akaunti ya Twitter ya ofisa habari wake, Kayleigh McEnany ilifungwa baada ya kusambaza habari hiyo ya New York Post.

"Kwa sababu anaripoti ukweli! Walifunga akaunti yake," alisema Trump.

Mtendaji mkuu wa Twitter, Jack Dorsey alieleza kusikitishwa kwa jinsi Twitter ilivyotoa taarifa ya jinsi ilivyoshughulikia habari hiyo.

"Maelezo yetu kuhusu tulichofanya katika habari ya @nypost hayakuwa mazuri. Na kuzuia usambazaji wa kutumia URL katika kutwiti au DM kukiwa hakuna chochote kuelezea kwa nini tulizuia, ni kitu ambacho hakikubaliki," alisema.

 

Advertisement