Tukutane kwa Mkapa

Muktasari:

Jamaa alifunga bao hilo pekee kwa shuti kali wakati mashabiki waliojaza Uwanja wa Mkapa wakiamini mechi ingeisha kwa suluhu na kuleta majonzi kwa Watanzania, na ghafla tu mabosi wa Jangwani wakamuibukia na kumalizana naye kabla ya kuachia picha za usajili wake.

KLABU ya Yanga imefanya usajili wa kushtukiza baada ya kumchukua mshambuliaji wa Burundi, Saidi Ntibazonkiza ikiwa ni ingizo jipya litakaloanza kuitumikia baada ya dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 16 na kufungwa Januari 15, mwakani.

Mshambuliaji huyo amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Yanga akitokea Vital’O ya kwao - saa chache tangu ang’are na timu yake ya taifa, iliyoicharaza Taifa Stars kwa bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopigwa Jumapili iliyopita.

Jamaa alifunga bao hilo pekee kwa shuti kali wakati mashabiki waliojaza Uwanja wa Mkapa wakiamini mechi ingeisha kwa suluhu na kuleta majonzi kwa Watanzania, na ghafla tu mabosi wa Jangwani wakamuibukia na kumalizana naye kabla ya kuachia picha za usajili wake.

Mara baada ya kusaini tu Mwanaspoti lilimuibukia na kufanya naye mahojiano maalumu, ambapo alifafanua juu ya usajili huo na safari yake kisoka barani Ulaya, na kukiri amesikia kejeli za mashabiki wa Simba “kwamba ni mzee”.

Saidi amesema uzee wake utajibiwa uwanjani na kuwataka Msimbazi wakutane naye Uwanja wa Benjamin Mkapa ndipo watajua ni mzee ama la, huku akifichua alichopanga kuifanyia Yanga atakapoanza kukipiga Jangwani. Endelea naye...!

USAJILI WA KUSHTUKIZA?

Ntibazinkoza anaelezea usajili wake ndani ya Yanga jinsi ulivyokuwa, unaweza kusema ni wa ghafla, lakini ukweli ni kwamba ulikuwa kwenye mipango kwa muda mrefu akisema kulikuwa na mazungumzo kwa muda mrefu nyuma na kufafanua; “Haukuwa uamuzi wa haraka kabisa, najua wengi watadhani kwamba uamuzi wa kusaini Yanga ni kama waliniona kwenye mechi ya Taifa Stars na Burundi pekee, hapana. Ni kama miezi miwili au mitatu nilikuwa katika mazungumzo na Yanga, ila kuna mambo yalikuwa hayajakaa sawa kwangu, niliwaomba wasubiri kidogo, lakini sasa nilipofika hapa wakakumbushia tena na nikaona nimalizane nao.”

USHAWISHI WA KAZE

Yanga usiku wa leo itampokea Kocha Cedric Kaze anayekuja kuifundisha na Ntibazinkoza anaelezea kocha huyo anavyomjua na alivyohusika katika dili lake la kutua Jangwani.

“Namjua kocha Kaze ni mtu wa nyumbani, lakini aliwahi kunifundisha timu ya taifa, alianza kunifundisha kuanzia mwaka 2011, tunajuana vyema na tunabadilishana sana mawazo na ni mtu ambaye tunazungumza sana hata kabla ya kuwa na mipango ya kuja Yanga,” anasema Ntibazonkiza.

“Nafikiri viongozi wa Yanga wanaweza kuliongelea sana hili, unajua Yanga kama nilivyokuambia walikuwa wananihitaji muda mrefu sasa sikujua labda wakati huo walikuwa wanaongea na Kaze! Ninachoweza kusema ni kwamba nilipofika hapa alinipigia akaniambia mambo kuhusu Yanga kuwa watanifuata niwasikilize na nikafanya hivyo.”

“Baada ya kusaini pia niliongea naye akanipongeza na kuniambia mipango yake ndani ya hii klabu na kwamba atakuja hapa siku sio nyingi. Nashukuru kwamba unasajiliwa, lakini pia unapata nafasi ya kufanya kazi na kocha unayemkubali na unayemfahamu vizuri na yeye anakufahamu, lakini pia hata kocha mwenyewe anakueleza kile ambacho anataka kutoka kwako kama mchezaji.”

KAZE ANAMTAKA NINI?

“Kifupi anataka mambo makubwa kutoka kwangu kwa kuwa anajua mimi ni mchezaji wa aina gani, anaujua ubora wangu na anajua naweza kuubadilisha mchezo dakika yoyote na kuipa timu matokeo, ameniambia kuna mambo tunatakiwa tuyafanikishe kwa pamoja kama timu na ni mmoja wa wachezaji atakayehitaji kufanya nami kazi kwa kukamilisha malengo ya klabu akitaka sana uzoefu wangu,” anasema Ntibazonkiza.

KOKOTE FRESHI

Baada ya kueleza hayo sasa anahamia nafasi ambazo anaweza kuzitumikia uwanjani na pia ni nafasi ipi amekuwa akipewa kisha anafanya vizuri

“Siku zote naweza kucheza nafasi zote pale mbele, iwe winga zote au hata namba 9 au 10, lakini mara nyingi nimekuwa nikitumika kucheza kama namba 10, naona wengi wanafurahia kazi yangu wakiniona nacheza hapo, ila sina tatizo kabisa kama nikipewa nafasi nyingine kati ya hizo,” anasema.

“Siwezi kusema hapa Yanga wanipe nicheze namba 10, lakini huo utakuwa ni uamuzi wa kocha ataamua anataka kunipa jukumu gani ili niitumikie klabu, kazi yangu ni kuifanya kazi hiyo kwa ufasaha na timu inufaike kwa ushindi.”

ULAYA HADI TANZANIA?

Ntibazonkiza kwa muda mrefu amecheza soka barani Ulaya katika nchi za Ufaransa, Kazakhstan, Uturuki na Uholanzi na anaelezea changamoto za kucheza nchi hizo ikiwa ni pamoja na uamuzi wa kurudi Afrika hasa Afrika Mashariki.

“Maisha ya kucheza Ulaya ni changamoto, kikubwa ni uvumilivu na unajua bahati nzuri nilienda kule nikiwa mdogo, kuishi Ulaya unatakiwa ujitambue na kujua kupanga mambo yako na uwe na malengo na binafsi sikuona tatizo lolote kikubwa ni jitihada,” anasema.

“Unakutana na wachezaji wakubwa uwanjani, nimeshindana na wachezaji wenye uzoefu mkubwa kama kina Neymar na wengine nikitanguliza malengo yangu binafsi na juhudi, ulikuwa ni wakati bora kwangu kuweza kushindana na wachezaji wenye majina namna hiyo.

“Ukiangalia utofauti kati ya huku Afrika na Ulaya ipo kubwa kule wanatumia akili sana na mbinu za kisasa, lakini hapa wanatumia nguvu ingawa natambua kwamba hata huku kuna vipaji vizuri.

“Umeniuliza kwanini nimerudi Afrika, nakumbuka nilirudi kujiunga na timu ya taifa baadaye ndio ikaja ile covid-19 na wakati huo kuna mambo mengi yakaibuka nikaona acha niangalie nafasi ya kuweka mwili wangu sawa unajua mimi ni mchezaji mkubwa siwezi kukaa tu bila kucheza, nikaona nitafute timu pale nyumbani ndio nikaenda Vital’O.”

KAVUMBAGU, TAMBWE

Baadhi ya mastaa wa Burundi ambao wamewahi kupita Yanga ni washambuliaji Didier Kavumbagu na Amissi Tambwe ambao walifanya makubwa katika klabu ya Yanga na hapa anaeleza alichoongea na wawili hao.

“Nawajua wote hao Tambwe na Kavumbagu nianze na Kavumbagu nakumbuka miaka ya nyuma niliwahi kuongea naye akawa akanieleza maisha ya hapa Yanga yalivyo, lakini wakati huo sikuwa na wazo la kuja kucheza hapa Tanzania. Pia wiki mbili zilizopita nilikuwa na Tambwe tulikuwa naye katika kambi ya timu ya taifa tunafanya mazoezi, nikamueleza juu ya huu mpango wa mimi kuja Yanga.

“Tuliongea mengi kuhusu mpira wa Tanzania, lakini pia aliniambia mengi juu ya maisha ya hapa Yanga na sioni sababu ya kuyaweka yote wazi lakini amenisaidia kujua mambo muhimu ambayo yatanisaidia wakati nafanya kazi hapa,” anasema.

ANAIZUNGUMZIAJE YANGA?

“Siwezi kusema Yanga ni timu ya aina gani kwa maana ya kikosi chao, nitakuwa muongo. Unajua ndio kwanza nimesaini mkataba hapa, lakini kiujumla hii ni moja ya klabu kubwa yenye mashabiki wengi Afrika, watu wake wanapenda mpira lakini pia naona viongozi wao wana malengo makubwa ya kutamani kuona hii timu inapiga hatua, nilipoona akili ya uongozi ipo hivyo nikashawishika kusaini hapa.”

JAMAA HANA NJAA

Akiwa Vital’O kama hujui ni kwamba Ntibazonkiza alikuwa pia akiisaidia kifedha klabu hiyo katika kuendesha mambo mbalimbali na hapa anaelezea akitangulia kucheka baada ya kuulizwa swali hilo.

“Ni kweli kuna mambo nilikuwa nasaidia pale, unajua hii ni klabu yangu ambayo naipenda tangu kwenye damu yangu na kabla ya kwenda Ulaya nilitokea hapo usisahahu niliporidi baada ya Covid 19 nilifikia hapo,” anasema.

“Kurudi kwangu Vital’O ni kama nilijisainisha mkataba tu hawakunipa kitu, niliamua mwenyewe kurudi pale niitumikie klabu yangu baada ya kuona siwezi kurudi tena Ulaya, nikiwa pale nilikuwa kama kocha, mchezaji na hata kiongozi na ndio hayo mambo ya kusaidia baadhi ya mambo ya kifedha katika uendeshaji nikawa nasaidia, sikuwa nalipa kila kitu kilichokuwa kinatokea ni kwamba kama kuna kitu naona naweza kusaidia na kufanya hivyo, siwezi kusema nilikuwa natoa kiasi gani ile ni klabu naiheshimu.”

UTUPIAJI MABAO

“Mimi naweza kufunga mabao ya aina mbalimbali nimeshafunga mabao ya vichwa, nimefunga na miguu yote, pia nimefunga ya mbali na hata karibu, kifupi najua kufunga ila hata kutoa pasi za mabao, pia hata mabao ya adhabu ndogo nafunga, ukinipa penalti nitafunga lakini itakuwa ngumu kusema mimi ni mtu wa mabao ya aina fulani,” anasema.

ANAJIANDAJE DERBY?

Ntibazonkiza anafahamu klabu kubwa zenye ushindani mkubwa nchini ni Simba, Azam na Yanga na hapa anaeleza alivyojipanga kiushindani hasa na Wekundu wa Msimbazi.

“Nafahamu hapa ushindani mkubwa ni wa Simba na Yanga, lakini kuna Azam ingawa hizo Simba na Yanga ndio zaidi, unajua ni kweli hizo ni timu kubwa hapa lakini siwezi kushtuka kabisa nitakapokutana na Simba, unajua nimecheza na upinzani na klabu kubwa duniani sioni kama Simba inaweza kuwa kubwa kuliko PSG ya Ufaransa au PSV ya Uholanzi, kuna wakati nimecheza dhidi ya Tottenham ya England,” anasema.

“Nafahamu kutakuwa na ushindani, hivyo kwangu ni kama changamoto mpya nimejipanga nayo na nitajiandaa, siwezi kushtuka nikisikia Simba labda washtuke kunisikia mimi, najua ikifika mechi hiyo mashabiki wa Yanga watahitaji ushindi, tutajiandaa kama timu Mungu akiwa upande wetu basi tutashinda.”

SIMBA ILIMTAKA BUANA

Simba iliwahi kumhitaji mshambuliaji huyu katika miaka ya nyuma na anaelezea kilichotokea na anavyoifahamu. “Simba nilikuwa naijua, unajua hapa na Burundi sio mbali, kwahiyo kuna wakati lazima utasikia kinachoendelea hapa, naijua Simba kama ambavyo naijua Yanga, ni kweli waliwahi kunihitaji miaka ya nyuma, lakini siwezi kueleza kwa undani kipi kilitokea, akili yangu sasa ni kuichezea Yanga kwa mafanikio makubwa hilo ndilo muhimu kwangu.”

KEJELI ZA SIMBA

Tangu Yanga imsajili Ntibazonkiza aliyezaliwa miaka 33 iliyopita mjadala umekuwa ni watani zao, Simba, kumuita “babu” wakilipiza kwa beki wao Joash Onyango aliyetangulia kutaniwa kama hivyo, lakini kumbe mshambuliaji huyo amesikia hilo na anasema:

“Nimesikia wananiita mzee nimecheka sana, unajua mimi sio kama wachezaji wengine ambao wanapenda kudanganya umri, hii ni miaka yangu halisi ambayo haijapunguzwa wala kuongezwa kwa kuwa nilienda Ulaya nikiwa mdogo nimependa watu wanavyosema mimi mzee.

“Ninachoweza kusema hapa naongea na wewe ni kwa vile umenifuata na nimeambiwa heshima yako kwa watu ambao uliomba nafasi ya kuongea nami, hao wanaoniita mzee waambie siku zote nitawajibu kuhusu hilo kupitia kazi yangu uwanjani. Inawezekana katika mechi ya Tanzania na Burundi, mimi ndiye nilikuwa mchezaji mwenye umri mkubwa, ila jiulize kuna kitu hao vijana uliona wananizidi?”

Je, unajua Ntibazonkiza anataka jezi ya staa gani ndani ya Yanga, fuatilia kesho.