Tulitaka kina Nape, Ngeleja, Makamba wafanye nini?

Tangu kuvuja kwa sauti mbalimbali za baadhi ya makada waandamizi wa CCM wakijadili mambo mbalimbali yaliyomhusisha mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania, John Magufuli, baadhi ya watu walianzisha mjadala kwa sababu wanasiasa wote waliohusishwa na sauti hizo wana historia ndani ya chama na ndani ya Serikali.

Sehemu kubwa ya wanamjadala walifurahia harufu ya mapambano ya waliosikika kwenye sauti hizo dhidi ya JPM na wanamjadala wengine walidhani kuwa sauti hizo zimeficha mkakati mzito wa kumhujumu Rais Magufuli na chama chake huku baadhi ya wanamjadala walitamani mvutano uliotokana na sauti hizo uwe mkubwa kupita kiasi ili Rais na serikali yake wapoteze mwelekeo.

Kila kundi lilikuwa na upande

Mathalani, viongozi na mashabiki wa vyama vya upinzani walitamani sana hisia za sauti zile ziwe hali halisi... sauti moja iliyowahi kurekodiwa ikihisiwa kuwa ni ya Waziri Mstaafu wa Mambo ya Nje iliwahi kunukuliwa ikisisitiza “CCM imeshavunjika na haipo tena”, hoja yake ikijikita kuelezea mtizamo wake kuwa Rais JPM haiongozi CCM sawasawa, jambo ambalo pia lilitafsiriwa kama hofu ya bure ya kiongozi huyo. Kundi la upinzani liliamini kuwa hisia za baadhi ya wana CCM waandamizi na kuvuja kwa sauti zao ni faida kubwa kwa upinzani hasa wakati wa kuelekea kwenye msimu wa chaguzi mbili zinazokuja; serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

Kundi la pili ambalo lilihusika sana na mjadala ni la ndani ya CCM ambalo kwa namna moja au nyingine, uongozi wa sasa wa CCM na Serikali yake, umezuia au kubana mirija ambayo kundi hilo liliitumia zamani na kujipa mamlaka ya kujimilikisha chama. Kundi hili lilifurahia sauti zile kwa sababu lilijua zikitokea na kuwa vitendo zingelipelekea uongozi wa CCM ulioko madarakani uyumbe na kupoteza mwelekeo na kwa sababu hiyo baadhi ya waandamizi wa kundi hilo wangelipata nafasi ya kupenya na kuongoza nchi.

Kundi la tatu ambalo lilihusika na mjadala ni la ndani ya CCM ambalo linaipigania CCM ibaki kuwa chama imara na kisichoyumbishwa, kundi hili ni la wanachama na viongozi waandamizi ambao wanaamini kuwa serikali ya awamu ya tano na CCM ya wakati huu vimejisahihisha na vinaendelea kujisahihisha sana, na kwamba vinahitaji muda, utulivu na kutobugudhiwa hasa na vijisiasa vya ndani ya chama ili kuvifanya vitekeleze azma na malengo ya CCM.

Msigano wa makundi yote haya wakati unaendelea, wahusika waliosikika katika sauti hizo waliendelea kukaa kimya na kujitafakari, huku makundi mjadala yenye upande yakiendelea kushikilia upande wake. Kwa kiasi kikubwa, katika makundi yote haya matatu kulikuwa na wanamjadala wengi ambao hawakutaka kabisa kuona madhara ya sauti zile yanatatuliwa, watu hao walitaka moto uwake na liwalo na liwe.

Ukomavu wa juu wa kisiasa

Jambo lilipokuwa limefikia, Nape na wenzake walipaswa kumtafuta Rais Magufuli na kumuomba radhi, na ndicho walichokifanya. Wengi wa wanamjadala hawakujua wanasiasa hao waandamizi walikuwa na fikra gani, wakadhani watajaribu kuendeleza mapambano ya kisiasa ya ndani ambayo kwa vyovyote wangelishindwa na wakadhani wangelichelewa sana kujirudi na kujishauri – walipojitokeza hadharani wakawaonesha wanamjadala kuwa wao walikuwa wanafikiri vizuri zaidi na mbele yao.

Uamuzi wa Nape, Makamba na Ngeleja kwa kiingereza unaitwa “political maturity” au kwa Kiswahili “ukomavu wa kisiasa”, uamuzi wa namna hiyo hushangaza watu wengi sana, kwamba mtu amewahi kutamka jambo fulani na likasikika kwa jamii kwa kukusudia au kutokukusudia, halafu mtu huyo anatafakari sana baadaye na kugundua kuwa fikra zake, msimamo wake au kile alichokuwa anakiamini siyo sahihi au hakina manufaa yoyote kwa taasisi yake, mhusika huyo anaamua kujirudi na kuachana na msimamo wa namna hiyo ambao hautakuwa na faida kwa jamii na taasisi yaani nchi na chama kinachoongoza dola. Kwa mtizamo wangu, Nape, Makamba na Ngeleja ni moja ya vijana waliofanya kazi kubwa ya kuitumikia CCM na Serikali yake; mwaka 2015 wakati nafanya uchambuzi wa wagombea urais kupitia CCM ambamo Makamba na Ngeleja walikuwa miongoni mwa waliochambuliwa katika safu za gazeti hili; kwenye eneo la sifa zao kuu wote wawili niliwaelezea kama wanasiasa wenye tija kubwa katika CCM na hasa nikionesha kuwa Makamba alikuwa na sifa za ziada zaidi ndani ya CCM ukilinganisha na vijana wengi sana wa ndani ya CCM na Tanzania.

Nape, kama ningelimchambua, ningempa sifa zake pia, kama kijana aliyejipambanua na kuipigania CCM muda wote katika maisha yake, huyu ni mwanasiasa kijana mwenye nguvu na ushawishi mkubwa sana, kokote kule ambako ungelienda kufanya shughuli za siasa, kama unampeleka Nape, utapata vijana wengi na watu wengi ambao watakuja kumsikiliza. Wote watatu, Nape, Makamba na Ngeleja ni wanasiasa wanaozika katika ngazi ya taifa na wana nguvu katika maeneo mkakati wanayotoka hasa katika ushawishi wa siasa za jumla. Mimi pia nina uzoefu wa kufanya siasa za upinzani kwa miaka 10 hivi, uzoefu huo unanionesha kuwa uaimara wa CCM ni mkubwa mno dhidi ya vyama vya upinzani, mitikisiko hii ya sauti zilizovuja za baadhi ya makada waandamizi wa CCM haifikii moja ya kumi ya mtikisiko ambao CCM iliupata mwaka 2015 na bado ikaumaliza salama, kwa hiyo kwa watu ambao wanazijua siasa za pande zote kama mimi walijua kuwa mtikisiko huo mdogo utapita bila shida, lakini ni muhimu kukiri kuwa vijana wa CCM ambao ni Nape, Makamba na Ngeleja wameonesha wao ni vijana wa kutegemewa na wenye fikra za kufikiria maslahi ya chama chao kuliko yao binafsi, hata pale wanapokuwa wameteleza.

Walichofanya vijana hawa watatu wa CCM kutambua wapo hawakutenda sawasawa na kuomba radhi ni ukomavu wa kipekee ambao umewapa uimara mpya ndani yao.

Lakini kubwa kuliko yote, kitendo cha Rais JPM kuwasamehe hadharani ni kitendo kikubwa na cha juu zaidi, kinaonesha namna CCM inavyotambua makosa ya vijana wake na inavyohitaji wapate muda wa kuyarekebisha ili wawe viongozi wazuri zaidi

Julius Mtatiro ni mkuu wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma. Ni Mtafiti, Mfasiri, Mwanasheria na Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Uchumi na Jamii. Simu; +25578753675. Barua Pepe; [email protected]