Tume ya walimu yamtaka Oluoch kuripoti kazini

Dodoma. Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imesema naibu katibu mkuu wa zamani wa Chama cha Walimu (CWT), Ezekiah Olouch anatakiwa kuripoti kwa mwajiri wake wa zamani ambaye ni Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Uamuzi huo umekuja siku chache baada ya Mahakama ya Rufani kutengua hukumu ya Mahakama Kuu iliyoridhia uamuzi wa katibu mkuu Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) kumuondoa mjumbe huyo wa Bunge Maalum la Katiba katika utumishi wa umma.

Katibu mkuu wa Utumishi aliamuru Olouch, ambaye ni mwalimu wa sekondari, kuondolewa katika utumishi wa umma mwaka 2017 kwa madai ya kushindwa kutekeleza masharti ya kuamua nani wa kumtumikia kati ya mwajiri wake ambaye ni Katibu wa TSC na CWT.

Akizungumza jana na Mwananchi, Katibu wa TSC, Winfrida Rutahindurwa alisema wanamtafuta Olouch ili wampe barua yake ya kurejeshwa kwa mwajiri wake wa zamani.

Alisema suala hilo ni nyeti na ndio maana wamekuwa wakimtafuta wampe barua.

“Kama utamuona, mwambie aje kuchukua barua yake,” alisema.

Alisema kama kwa mwajiri wake kuna hatua nyingine za kuchukua, basi zitafuata baada ya kutekeleza hilo.

Akielezea chanzo cha mgogoro huo, Winfrida alisema Olouch aliomba likizo bila malipo kwa ajili ya kwenda kufanya kazi CWT na muda wake ulipomalizika aliomba kuongezewa.

Hata hivyo, alisema Serikali ilikataa na kumtaka kwenda kuripoti kwa mwajiri wake wa zamani, jambo ambalo hakukubaliana nao.

“Kule aliazimwa tu kwa kupewa likizo isiyokuwa na malipo. Sasa alimaliza na kuomba tena, lakini Serikali ilikataa. Ukiomba likizo bila malipo Serikali inaweza kukupa ama kutokupa,” alisema.

Olouch alipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo, hakupatikana.

Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili Februari 12, Olouch alisema tayari amewasilisha barua katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya CWT Januari 28 hadi 30 mwaka huu kuwajulisha kuwa sababu zilizomuondoa zimetenguliwa na Mahakama ya Rufaa.

Majaji watatu waliosikiliza shauri lake, waliafikiana kuwa katibu wa TSC aliyemfukuza kazi hakuwa na mamlaka hayo na kama alikuwa na sababu zozote kuwa Oluoch alifanya kosa, angemripoti.