Tundu Lissu: Nimepona, situmii magongo wala dawa

Muktasari:

Aliyewahi kuwa Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema kuanzia jana Jumanne hatumii tena dawa wala magongo kutembea na baada ya Agosti 20, 2019 atakuwa tayari kurejea nchini mwake kutoka Ubelgiji aliko sasa.

Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Tundu Lissu amesema amehitimisha matumizi ya dawa alizoanza kuzitumia tangu Septemba 7 mwaka 2017.

Lissu alianza kutumia dawa hizo Septemba 7 mwaka 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma ambapo tangu wakati huo amekuwa akipatiwa matibabu nje ya nchi.

Katika salamu kwa marafiki zake alizozitoa leo Jumatano Julai 31, 2019, Lissu ameanza kwa kuzungumzia afya yake akisema, “Leo Julai 31, 2019 ni siku ya kwanza tangu niliposhambuliwa Septemba 7, 2017, situmii dawa ya aina yoyote.”

“Kwa maelekezo ya madaktari wangu, jana (Jumanne) ilikuwa siku ya mwisho ya mimi kutumia dawa ambazo nimezitumia tangu siku niliposhambuliwa,” amesema mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki.

“Na jana hiyohiyo nilitimiza mwezi mzima tangu niache kutumia magongo. Ijapokuwa bado nachechemea kwa sababu ya goti kutokukunja sawasawa, sasa ninatembea bila msaada wa magongo,” amesema

Katika salamu zake, Lissu amesema, “Safari yangu na yetu, ndefu ya matibabu itakamilika Agosti 20,2019 nitakapokutana na timu ya madaktari wangu kwa ajili ya vipimo vya mwisho na ushauri. Baada ya hapo itakuwa ni maandalizi ya kurudi kwetu. Hakutakuwa na sababu tena ya kitabibu ya mimi kuendelea kukaa Ulaya.”

Amesema kwa vile tumekuwa pamoja kwenye safari hii ndefu, hatuna budi kupongezana na kumshukuru Mungu kwa hatua hii nzuri nilikofikia.

“Mimi na familia yangu hatutachoka kuwashukuru sana kwa kuwa pamoja nasi katika kipindi chote hiki kigumu. Mungu awabariki sana.”

Jambo la pili ambalo Lissu amelizungumzia ni lile la kupoteza sifa ya kuwa mbunge baada ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kulieleza Bunge hilo Juni 28, 2019 kuwa Lissu amepoteza sifa hizo kwa sababu mbili.

Spika Ndugai alisema sababu hizo ni kutokujaza fomu za mali na madeni kwa viongozi wa umma na kutokutoa taarifa kwake ya wapi  alipo.

Lissu amesema  tangu alipopoteza ubunge, “sijasema maneno mengi sana, zaidi ya kusema kwamba tutaenda Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo.”

“Kesi za ubunge, kama zilivyo kesi zote za uchaguzi wa kisiasa, ni kesi za kisiasa. Ni mwendelezo wa mapambano ya kisiasa katika uwanja tofauti. Kwa sababu hiyo, ni kesi nyeti na za kipekee sana. Zinahitaji umakini mkubwa katika kuziandaa na kuziendesha. Nina uzoefu mkubwa nazo, kwa sababu nimezifanya sana tangu 2005.”

“Sasa ninaweza kuwafahamisha kwamba mimi na timu ya mawakili wangu tuko tayari kuingia Mahakama Kuu ya Tanzania. Tutafanya hivyo muda wowote kuanzia leo. Maandalizi yote yanayohitajika yamekamilika,” amesema Lissu

Amesema tunataka kuiomba Mahakama Kuu itoe jibu la swali alilouliza Spika Ndugai na walio nyuma yake: je, Spika wa Bunge la Tanzania ana uwezo kikatiba na kisheria wa kufuta ubunge wa mbunge yeyote yule, kwa sababu yoyote ile, bila kumuuliza mbunge husika jambo lolote kuhusu sababu za kumfuta ubunge huo???

“Nitawajulisheni mara moja kesi hii itakaposajiliwa rasmi. Kama itawapendeza, nitawaomba mtakaopata nafasi kuhudhuria mahakamani, kwa niaba yangu, wakati wote kesi hiyo itakapokuwa inaendelea,” amesema