Tundu Lissu akwamisha kesi yake kuendelea

Muktasari:

  • Mdhamini wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, Ibrahimu Ahmed, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa mshtakiwa huyo bado anaendelea kupatiwa matibabu nje ya nchi.

Dar es Salaam. Mdhamini wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa mshtakiwa huyo bado anaendelea kupatiwa matibabu nje ya nchi.

Mdhamini huyo, Ibrahimu Ahmed, ameieleza mahakama hiyo leo Jumatatu  Septemba 23, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Lissu na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Ahmed  amedai kuwa Lissu bado ni mgonjwa na anaendelea na matibabu.

Lissu, yupo nje ya nchi kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi, Septemba 7 mwaka 2017 akiwa  katika makazi yake jijini Dodoma.

Kabla ya Ahmed kueleza hayo, wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa, hivyo kutokana na mshtakiwa mmoja kuwa mgonjwa, aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 23, 2019  itakapotajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai namba 208/2016 ni Mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili wanadaiwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa, Januari 13 ,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Mehboob pia anadaiwa kuwa alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.