UDHIBITI NDANI YA CHAMA: Membe hatarini CCM

Dar es Salaam. Bernard Membe, mmoja kati ya wagombea urais walioonekana tishio mwaka 2015, anaweza kupitia njia ngumu zaidi ya ile aliyopitia wakati wa kuelekea uchaguzi huo mkuu.

Wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, Membe pamoja na Edward Lowassa, Frederick Sumaye, Steven Wasira, William Ngeleja na January Makamba waliitwa mbele ya Kamati ya Maadili ya CCM kuhojiwa.

Kipindi hicho, Membe na wenzake walitiwa hatiani kwa makosa ya kuanza mapema kampeni za kuusaka urais wa 2015 kabla ya muda uliowekwa na chama hicho na hivyo kuzuiwa kujihusisha na shughuli za chama hicho, ikiwa ni pamoja na kugombea uongozi, kwa kipindi cha miezi 12.

Kipindi hicho kiliisha kabla ya harakati za uchaguzi wa ndani ya CCM kuanza na hivyo kuwapa fursa kugombea nafasi walizotaka.

Safari hii, hali inaweza kuwa mbaya kwa Membe, ikiwa imesalia miezi michache kabla ya kuanza kwa harakati za kugombea uongozi kwa tiketi ya chama hicho kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Adhabu yoyote au uamuzi kama wa mwaka 2014 wa kumuweka chini ya uangalizi kwa kipindi kama hicho, itazuia uwezekano wa kuhusika katika uchaguzi wa mwakani, kama atakuwa na nia ya kujitokeza kupambana na Rais aliye madarakani, tofauti na utamaduni wa chama hicho.

Juzi, Halmashauri Kuu ya CCM iliagiza Membe, ambaye amekuwa hana uhusiano mzuri na uongozi wa juu wa chama hicho, pamoja na Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana kufika mbele ya kamati hiyo ya usalama na maadili.

Watatu hao wameitwa katika kipindi ambacho sauti zao zilisambaa katika mitandao ya kijamii zikizungumzia kupasuka kwa CCM kwa kiwango ambacho hakiwezi kuungika na wakati fulani wakilaumu uongozi kwa kusababisha hayo.

Makamba na Kinana, ambao waliwahi kushika nafasi nyeti ya kuwa watendaji wakuu wa CCM, pia wameitwa ukiwa umepita muda mrefu baada ya kuandika barua ya kulalamikia uongozi kutochukua hatua dhidi ya mtu ambaye alikuwa akiwadhalilisha katika vyombo vya habari na kumtuhumu kuwa mtu huyo analindwa na mwenye mamlaka.

Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema katika taarifa yake kuwa kamati hiyo itawahoji watatu hao dhidi ya tuhuma zinazowakabili.

Lakini Membe anaweza kukumbana na mambo matatu kwa mujibu wa kanuni za chama hicho ambayo ni kurekebishwa, kuondolewa katika chama au kuvuliwa uongozi.

Licha ya kuwa adhabu hizo zinaweza kuwakumba wote ikiwa watakutwa na hatia, Membe ndio anaonekana kuwa ataathirika zaidi kutokana na kuwa itakuwa ni mara ya pili kuadhibiwa na kamati hiyo tofauti na wenzake. Membe pia anatajwa kuwa katika mbio za urais, ingawa hajawahi kuzungumzia hilo.

Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally aliwahi kusema Membe amekuwa akikwamisha kampeni za urais za mwaka 2020 na hajawahi kwenda ofisini kwake.

Membe amesema anasubiri kwa hamu wito huo. Lakini wasomi wanaliangalia suala hilo kwa mtazamo tofauti.

“Hatua hiyo isichukuliwe kama ni kesi ambayo wastaafu hao wanakwenda kujibu, bali uwe ni mkutano wa kutafuta suluhu,” anasema mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda.

“Kwanza naona kama imechelewa sana. Yale matukio yalivyotokea kama vile sauti (za simu) ilitakiwa chama kiwe kimeshawakutanisha, wanaongea wanayamaliza. Naamini likiongelewa litaisha kwenye chama na wataendelea kukumbushana kwamba kuna njia maalumu za kufikisha malalamiko.

“Kama wakiwaita ikawa kesi, watatoka kule wakiwa na manung’uniko zaidi na italeta picha mbaya. Wakiitwa kwa vitisho ni dhahiri kwamba haitakuwa sawa.”

Mbunge wa zamani, Njelu Kasaka ameeleza kushangazwa na kitendo cha walalamikaji kugeuzwa kuwa washtakiwa. “Walitoa tamko la malalamiko kwa wanaodai kuwa makada wa chama, kwa hiyo halikupaswa kwenda kisiri siri, wakaliweka hadharani. Suala lao sasa limepuuzwa badala ya kuwa walalamikaji, sasa wamegeuzwa kuwa walalamikiwa,” alisema Njelu Kasaka, mwanasiasa mkongwe nchini.

“Sina hakika kama itasababisha mpasuko zaidi, lakini ni vema likawekwa katika uwazi na ukweli uendelee kudumishwa. Kuna matamshi yamewahi kutolewa na watu wanaodai kuwa makada wa CCM, lakini sijasikia wamechukuliwa na chombo chochote. Ni vizuri kuangalia tunaelekea wapi.”

Hata hivyo, Kasaka alisema utaratibu wa kuwaita wanachama kwenye kamati za maadili ni mzuri kwani unakirejesha chama kwenye mstari bila kujali ngazi ya wanachama aliyeitwa.

Mwingine aliyezungumza na Mwananchi ni Profesa Bakari Mohamed, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm).

“CCM iwe makini na hatua hiyo kwa kuwa inaweza kuiweka sehemu mbaya,” alisema Profesa Mohamed.

Alisema viongozi hao watatu hawakuomba msamaha kwa kuwa hawana cha kupoteza ndani ya chama hicho kama ilivyokuwa kwa wabunge watatu--January Makamba, Nape Nnauye na William Ngeleja.

Wabunge hao watatu, ambao pia sauti zao zilisikika katika mazungumzo ya simu wametangaziwa msamaha na Halmashauri Kuu ya CCM baada ya kuomba radhi na kutakiwa kutorudia vitendo hivyo.