UDSM waanzisha shahada ya uzamili sayansi ya takwimu

Wednesday December 4 2019

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeanzisha shahada ya uzamili ya sayansi ya takwimu na kuwa chuo pekee Afrika Mashariki kutoa shahada hiyo.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Desemba 4, 2019  jijini Dar es Salaam na Mkuu wa shule ya Tehama (CoICT) katika chuo hicho, Dk Mussa Kisaka wakati wa ufunguzi wa tamasha la data chuoni hapo.

Dk Kisaka amesema lengo la kuanzisha shahada hiyo ni kuongeza uelewa zaidi wa masuala ya takwimu na jinsi zinavyoweza kutumika kufanya uamuzi wa maendeleo ya watu binafsi, mashirika na Taifa.

"Huko nyuma tulikuwa tunatoa kozi fupi za masuala ya data lakini tukaona kuna haja ya kuanzisha shahada hii  ambayo ni ya kwanza kutolewa hapa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla," amesema.

Amesema tamasha la 2019 linalenga kuongeza hamasa kwa wanawake kushiriki katika masomo ya sayansi ili wawe na uwezo mkubwa wa kuzitafuta na kutumia takwimu katika mambo mbalimbali.

Akifungua tamasha hilo, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Inni Patterson amesema nchi yake iko tayari kufadhili kazi za ubunifu zinazofanywa na Watanzania katika kutatua changamoto mbalimbali.

Advertisement

 

Amesema lengo ni kumwinua Mtanzania ili aweze kuondokana na changamoto za maisha na kujiletea maendeleo. Amesema wanafuata kauli ya Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliwahi kusema, "maendeleo ya kweli ni ya watu, siyo ya vitu."

 

"Data Lab ni taasisi ambayo inawekeza kwa watu, na sisi tunaunga mkono ubunifu unaofanywa na watu, hatupendi kusikia kuhusu changamoto hizo ziko kila mahali. Tunataka kuona unafanya kitu kuondoa hizo changamoto, hapo ndipo sisi tunakusaidia," amesema Patterson.

 

Advertisement