VIDEO: UPDP yaungana na vyama vingine vinne vya upinzani kususia uchaguzi wa serikali za mitaa

Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa akizungumzia na wanahabari leo.

Muktasari:

UPDP yaungana na vyama vya Chadema, ACT- Wazalendo, Chauma na NCCR-Mageuzi, kujiondoa katika uchaguzi wa serikali za mitaa  utakaofanyika Novemba 24, 2019 wakitaka mchakato uanze upya badala ya kuwarudishwa

Dar es Salaam. Chama UPDP, kimeunga na vyama vya Chadema, ACT- Wazalendo, NCCR- Mageuzi na Chaumma kuwataka wagombea wake kujitoa katika mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019, licha ya Serikali kuamuru wagombea wote waliochukua na kurejesha fomu kushiriki mchakato huo.

Kwa nyakati tofauti vyama vya ACT- Wazalendo, Chadema, Chaumma,  NCCR - Mageuzi vilitangaza kujitoa katika uchaguzi huo kwa kile walichodai kutoridhisha na mwenendo wake ikiwemo wagombea wa upinzani kuenguliwa.

Lakini jana Jumapili, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo alisema Serikali imeamuru wagombea wote waliochukua fomu na kurejesha kushiriki mchakato huo, akisema hakuna mpira kuwekwa kwapani badala yake wakutane kwenye sanduku la kura.

Leo Jumatatu, Novemba 24, 2019 Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa amezungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu hatua ya Serikali kuwaruhusu wagombea waliochukua na kurejesha fomu kushiriki uchaguzi huo.

"Hatua ya Jafo kuwarudisha wagombea wote haina uzito wowote. Waziri alipaswa kuwachukua hatua wasimamizi wasaidizi ambao wamevuruga mchakato huu na kusababisha sintofahamu.”

"Angeonyeshwa kukerwa vitendo vilivyofanywa na wasimamizi wasaidizi kwa kuchezea amani ya nchi ya kuwaengua wagombea wa vyama upinzani,” amesema Dovutwa

“UPDP tunatoa wito kwa wagombea wetu kutoshiriki uchaguzi huu labda mchakato uanze upya  kwa sababu hatutapa haki chini ya kanuni na sheria zilezile zinazowapa kiburi wasimamizi wasaidizi " amesema Dovutwa

Dovutwa ametumia nafasi hiyo kuwataka viongozi wa vyama vya upinzani kuwa watulivu ili kupata muda wa kutafakari zaidi kadhii ya iliyojitokeza katika mchakato wa uchaguzi huo.