USHAURI WA DAKTARI: Athari za woga kabla ya kujamiiana

Woga kabla ya kujamiiana ni tatizo ambalo linaweza kuwatokea wanaume katika kipindi cha maisha yao na kuwasababishia kushindwa au kushiriki tendo hilo chini ya kiwango na wenza wao.

Ni tatizo ambalo likimpata mtu mara kwa mara linaweza kuwa chanzo cha kupata tatizo la kuwahi kufika kileleni, kushindwa kuendelea mizunguko mingine ya tendo au kukosa hamu ya tendo.

Tatizo hili linapomkabili mwanaume inaweza kuwa chanzo cha kuvunjika mahusiano au kuleta mifarakano. Mwanaume anaweza akaonekana mtulivu na anayeongea kuliko mwanamke lakini ndani ya mioyo yao huwa na hofu hali inayomfanya kuwa mwoga hasa nyakati za matayarisho kabla ya tendo.

Yafuatayo ni mambo mbalimbali yanayompa hofu mwanaume na kumfanya kuwa mwoga.

Hofu ya kuwa hanithi (Impotence) ndio tatizo linaloongoza kuwafanya wanaume wapate woga wa kujamiiana na wenza wao. Machapisho mengi ya kitabibu yanaonyesha karibu asilimia 90 ya wanaume wenye tatizo la kushindwa kusimika husababishwa na matatizo ya kisaikolojia na huku 10 huwa ni ya kibaiolojia.

Hofu ya maumbile madogo ya kiume ni mojawapo ya tatizo linalochangia woga, hupata dhana kuwa atashindwa kukidhi hisia za mwenza wake. Wanaume wengi wanashindwa kufahamu kuwa umbile dogo si chanzo cha kushindwa kumridhisha mwenza.

Mwanamke anaweza akaridhishwa na kufika keleleni hata kwa uume wenye saizi ya kidole cha mtu mzima.

Hofu ya tatu ni tatizo la kuwahi kufika mshindo kabla ya kumridhisha mwenza, humweka mwanaume katika mawazo na kumfanya kuwa mwoga, akihisi kuaibika kwa kutotimiza wajibu wake.

Baadhi ya wanaume huweza kujihisi kuwa hawako kawaida wanapojilinganisha na wanaume wengine, hususani wanapowasikia wakijisifu kuwa na maumbile makubwa, uwezo wa kwenda mizunguko mingi bila kuchoka huwasababishia hofu isiyo na lazima.

Hofu ya kuporwa mwenza, inawatawala wanaume kwa kiasi fulani na kuwajengea woga pale anapokuwa anajiandaa kwa ajili ya tendo. Hofu hii hutokana na namna mwanaume anavyompenda mwenza wake na kuvutiwa naye, hudhani na wengine huwa na hisia kama zake. Huanza kupata wivu ambao baadaye huwa na zao la kuwa na hofu mwishowe woga mkali.

Maumbile ya mwanamke yameumbwa kiasili kuwa na mvuto wa kipekee kiasi kwamba baadhi ya wanaume anapomwona mwenza wake hupatwa na hofu ya maumbile hayo, hivyo kupata woga kabla ya kushiriki tendo.

Kwa wanaume ambao tayari wameshaingia katika ndoa na waaminifu huwa mara nyingi wanapata hofu ya kukosa udhibiti wa hisia zao za kimwili, ikiwamo kushindwa kujizuia kutamani wanawake wengine.

Ni jambo ambalo kisayansi inakubalika kuwa mwili wa mwanaume huwa na matamanio na kuamsha hisia zake haraka pale anapoona mwanamke mwenye mvuto.

Hofu inaibuka pale anapokosa udhibiti wa hisia zake za kimwili na kujikuta akitamani wanawake wengine. Mwanaume hujikuta anapata hofu hasa anapojiona ni mkosefu kwa kuvunja uaminifu katika mahusiano au ndoa.

Haya ni baadhi ya mambo ambayo mara kwa mara yanachangia mwanaume kuwa na hofu ambayo huzaa woga uliopitiliza kabla ya kujamiiana.

Woga unaingilia mtiririko mzima wa mwanaume kupata msisimko na kufika kileleni, hivyo kuwafanya kupunguza hamu au kushindwa kutamani tendo, au kufika mshindo haraka kabla ya kuwaridhisha wenza wao.