Ubadhilifu wawatupa nje vigogo wa CCM Wilayani Ulanga

Mwenyekiti wa CCM mkoa Morogoro Innocent Kalogeris akiteta jambo na Katibu wa CCM huo Shaka Hamdu Shaka  wakati wa kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Morogoro jana ambacho kimewavua uongozi viongozi 9 wa halamshauri Wilaya Ulanga.

Muktasari:

Sakata la ubadhilifu wilayani Ulanga limekwenda na Mwenyekiti na Makamu mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo.  Chama kimedai walishindwa kutekeleza majukumu yao na kusimamia maadili ya uongozi

Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi(CCM) kimewavua uongozi viongozi wa chama hicho wilayani Ulanga baada ya kubainika kuwa na hatia katika sakata la  ubadhilifu.

Uamuzi huo ulifikiwa usiku wa jana katika kikao cha halmashauri kuu ya CCM mkoani Morogoro, Tanzania kilichokuwa na ajenda mbalimbali ikiwemo ya kujadili hatma ya viongozi hao baada ya kuonekana kuwa na hatia katika ubadhirifu huo.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro Shaka Hamdu Shaka amewataja waliovuliwa nafasi hizo ni  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Ulanga Furaha Lilogeri, Makamu Mwenyekiti Amina Seif na wajumbe  saba wa kamati ya mipango na Fedha wa halmashauri hiyo.

Amesema CCM kama chama chenye dhamana kiliamua kuchukua hatua kwa viongozi hao baada ya kubainika kwa namna moja au mwingine kuwa walihusika.

Shaka ameeleza kuwa  halmashauri kuu ya mkoa huo  imejiridhisha kuwa viongozi walishindwa kusimamia dhamana waliyopewa na wananchi na CCM  kwa ujumla katika kusimamia majukumu yao.

“Septemba mwaka huu Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa alifanya ziara katika mkoa wa Morogoro na kubaini ubadhirifu mkubwa wa fedha za serikali ambapo Ded wa Ulanga aliondolewa na kuagiza watumishi wote waliohusika wachukuliwe hatua,   CCM tulimuahidi waziri mkuu kuwa hatutasita kuchukua hatua kwa viongozi wake waliohusika. 

“Hawa tumeona wamekiuka  maadili ya uongozi kwa kutumia vibaya dhamna waliyokabidhiwa na wananchi kwa niaba ya wananchi hivyo hatuna budi kuwaondoa kwenye nafasi hizo,” amesema Shaka