Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia mikononi mwa Takukuru

Muktasari:

Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania imekabidhiwa jalada na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki la uchunguzi la upotevu na matumizi mabaya ya fedha katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia.

Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeikabidhi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) jalada la kulifanyia uchunguzi upotevu wa fedha katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Faraji Mnyepe amekabidhi jalada hilo leo Ijumaa Novemba 15, 2019 kwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo katika ofisi ndogo za wizara jijiji Dar es Salaam.

Hatua hiyo imekuja kutokana na jitihada za Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais John Magufuli za kupambana na kuzuia rushwa pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Uchunguzi huo unafanyika baada ya kubainika upotevu/matumizi mabaya ya fedha katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia.

Kuhusu kiwango cha fedha kilichopotea Katibu Mkuu, Dk Mnyepe amesema kitajulikana mara baada ya Takukuru kukamilisha uchunguzi huo wa jalada walilokabidhi.