Uchakavu wa vifaa vya kuongoza ndege yatajwa kuwa changamoto Afrika

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari

Muktasari:

Wadau mbalimbali wa usafiri wa anga kutoka bara la Afrika na wengine kutoka mabara mengine wamekutana jijini Dar es Salaam nchini Tanzania kujadili namna ya kuboresha huduma za sekta hiyo.

Dar es Salaam. Uchakavu wa vifaa vinavyotumika kutoa huduma za uongozaji wa ndege umetajwa kuwa changamoto inayoikabili sekta hiyo muhimu barani Afrika.

Hayo yamesema leo Jumanne Septemba 3, 2019 na wadau waliohudhuria mkutano wa wadau wa huduma za anga na uongozaji wa ndege wa Afrika unaoendelea Tanzania chini ya uratibu wa baraza la Canso la Afrika.

Mwenyekiti wa Canso Afrika ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari amesema kupitia mkutano wa sekta ya anga ndani ya bara la Afrika inaweza kutatua changamoto zinazoikabili huku akisisitiza ushirikiano.

"Hapa tutajadili masuala ya usalama, miundombinu, mafunzo na teknolojia lakini ufanisi wa sekta hii unategemea ushirikiano, kupitia ushirikiano tunaweza kutatua changamoto zinazotukabili," amesema Johari.

Amesema unahitaji mfumo uliopo sawa katika uongozaji wa ndege katika nchi zote ili ndege inapotoa bara lingine kuja Afrika ipate huduma bora ya viwango sawa katika nchi zote itakazokatiza anga lake.

Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo amesema sekta ya usafiri wa anga ni sekta muhimu katika ukuaji wa sekta nyingine katika nchi na Serikali ya Tanzania itaendelea kuwekeza katika sekta hiyo.

"Tunaendelea kuboresha sekta kwa kuboresha miundombinu na ununuzi wa ndege za Serikali, sekta ya usafiri wa anga ni muhimu kwa ukuaji wa sekta ya utalii, watalii wengi wanatumia ndege. Kuongezeka kwa abiria na idadi ya ndege ni ishara kuwa sekta inakwenda vizuri na umuhimu wa Canso unadhihirishwa na uchache wa ajali," amesema Kamwelwe.

Mkurugenzi Mtendaji wa Canso, Simon Hocquard amesema kuna viashiria vya sekta ya usafiri wa anga katika bara la Afrika kukua kwa kiasi kikubwa katika siku zijazo.