Ufaransa, Ujerumani waridhishwa na matumani makubaliano Brexit

Muktasari:

  • Viongozi wa nchi hizo wanatarajiwa kukutana leo na Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson mjini Brussels, Ubelgiji katika mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi za Umoja huo.

Brussels, Ubelgiji. Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel wameelezea matumaini ya kufikiwa makubaliano baina ya Umoja wa Ulaya (EU) na Uingereza kuhusu mchakato wa Brexit.

Hatua hiyo imekuja siku moja kabla ya viongozi hao kukutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson katika mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi za Umoja huo uliofanyika mjini Brussels, Ubelgiji.

 Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Kansela Merkel jana Jumatano Oktoba 16, Rais Macron alisema anaamini kwamba makubaliano hayo yatahitimishwa haraka leo.

Kwa upande wake Kansela Angela Merkel alisema mazungumzo baina ya Umoja huo na Uingereza yalikuwa katika hatua za mwisho na kuongeza kuwa habari anazozipata kutoka Brussels yanakofanyika mazungumzo hayo zilikuwa za kutia moyo.

Awali kiongozi wa mazungumzo hayo upande wa Umoja huo, Michel Barnier alisema muafaka umepatikana kuhusu masuala yote makuu ingawa bado vipo vipengele ambavyo havijapatiwa ufumbuzi.