Uhaba wa madarasa watesa wanafunzi 2,750 Tarime

Sunday February 23 2020

By Beldina Nyakeke Mwananchi [email protected]

Musoma. Zaidi ya wanafunzi 2,750 wa shule za Msingi Kewanja na Nyamongo katika wilaya ya  Tarime mkoani Mara wanalazimika kutumia vyumba vya madarasa 11 kutokana na upungufu wa madarasa unaokabili shule hizo.

Shule hizo zililazimika kuunganishwa baada ya shule mama ya Nyamongo kuzidiwa wanafunzi hivyo ikalazimu uongozi wa kijiji kwa kushirikiana na halmashauri kuanzisha shule nyingine ya Kewanja ndani ya shule hiyo.

Akizungumza kwenye kongamano la wadau wa elimu mjini hapa leo Jumapili Februrari 23, 2020, mwenyekiti wa kamati ya shule ya Kewanja, Joseph Chacha amesema kutokana na kutokuwapo kwa madarasa ya kutosha uongozi wa shule hizo mbili ulikubaliana kuwa wanafunzi wa shule zote mbili kutumia madarasa hayo kwa awamu mbili tofauti kwa siku.

Amesema kuwa hali hiyo imekuwa ikiathiri utoaji wa elimu kwa wanafunzi kwa vile wanalazimika kusoma kwa saa chache tofauti na sera ya elimu nchini.

Amesema kuwa umefika muda sasa tatizo la upungufu wa miundombinu ya madarasa kwa shule hizo kupatiwa ufumbuzi wa kudumu ili wasome katika mazingira rafiki.

Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Kewanja, Baby Tambuko amesema shule yake ilianzishwa mwaka 2013 lakini tangu muda huo, wanatumia madarasa ya shule mama ya Nyamongo.

Advertisement

 

Amesema kutokana na upungufu wa madarasa 21 unaoikabili shule hizo, wanafunzi wanalazimika kusoma kwa awamu mbili, ya kwanza inaanza saa 1.20 asubuhi hadi saa 6.20 ili kupisha awamu ya pili.

“ Hata hivyo tumekubaliana madarasa ya mitihani yaani la nne na la saba wao wanasoma siku nzima kwa kubanana hivyohivyo ili waweze kwenda sambamba na wenzao,” amesema mwalimu huyo

 

Advertisement