Uhaba wa maji Arusha kumalizika Novemba

Wednesday September 11 2019

By Mussa Juma, Mwananchi [email protected]

Arusha. Uhaba wa maji ambao unalikabili Jiji la Arusha nchini Tanzania unatarajiwa kumalizika kuanzia Novemba 2019 kutokana na kukamilika kazi ya uchimbaji visima viwili virefu ambavyo vinatoa maji lita zaidi ya 60 milioni kwa siku.

Mahitaji ya maji katika Jiji la Arusha ni lita 94 milioni kwa siku ambazo zinazalishwa kwa sasa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (AUWSA) ni lita 40 milioni hivyo ongezeko la lita 60 milioni linakuja kumaliza tatizo la maji katika Jiji hilo.

Mkurugenzi mkuu wa AUWSA, Luth Koya ametoa taarifa hiyo leo Jumatano Septemba  11,2019 kwa kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Arusha wakati akitoa taarifa za utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji, katika Jiji hilo utakaogharimu kasi cha Sh520 bilioni ambazo zimetolewa na Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Koya amesema katika mradi huo ambao ulizinduliwa na Rais Magufuli Desemba 2, 2018, tayari visima 11 kati ya 56, vimechimbwa na ulazaji bomba umefikia asilimia 19, muundo wa mradi umefikia zaidi ya asilimia 30 na tayari ujenzi wa matanki ya kuhifadhi maji umeanza.

"Mradi mzima ukikamilika tatizo la maji litakuwa limekwisha katika jiji la Arusha, lakini pia vijiji vyote vya wilaya za Arumeru na Simanjiro, ambapo mradi utapita zitapata huduma ya maji," amesema.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo na kutaka AUWSA kuhakikisha ifikapo Novemba 2019 baadhi ya maeneo yaanze kupata maji.

Advertisement

Gambo alitaka AUWSA, kuhakikisha  inaondoa changamoto ya maji katika maeneo ambayo yanashida ya maji hata kabla ya kukamilika mradi mkubwa wa maji mwakani.

Mwenyekiti wa  CCM wilaya ya Arusha, Joseph Masawe licha ya kupongeza AUWSA kwa mradi huo ametaka mamlaka hiyo kutoa taarifa za mara kwa mara hasa juu ya mgao wa maji kwa sasa lakini pia  kumaliza changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza.

"Kuna tatizo la kukatika maji muda mrefu baadhi ya maeneo, lakini pia bomba kukatwa kutokana  na ukarabati wa barabara tunaomba mshughulikie matatizo haya,” amesema

Advertisement