Uhakiki vyama vya siasa wawaibua wanasiasa, Mutungi awajibu

Msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania, Jaji Francis Mutungi

Muktasari:

Vyama vya siasa vitaanza kufanya uhakiki kuanzia Machi 27 hadi Aprili 20, 2020 licha ya Msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania, Jaji Francis Mutungi kukiri vinapitia hali ngumu.

Dar es Salaam. Vyama vya siasa vitaanza kufanya uhakiki kuanzia Machi 27 hadi Aprili 20, 2020 licha ya Msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania, Jaji Francis Mutungi kukiri vinapitia hali ngumu.

Mutungi ameyasema hayo leo Jumanne Machi 10, 2020 alipokutana na viongozi wa vyama vya siasa kuelezea umuhimu wa uhakiki huo ikiwa ni pamoja na kuwa na fursa ya kuelezea changamoto zinazowakabili.

Amesema kutokana na hali ngumu baadhi ya vyama vimeomba kusogezwa kwa muda wa uhakiki lakini amesisitiza uhakiki huo ufanyike katika muda huo.

“Mimi kama msajili mnaniita mlezi wenu nitaendaje kwenye uongozi serikalini kusema vyama vina shida hii kwa kigezo ni kipi? Ni kwa kigezo cha uhakiki niliofanya,” amesema Mutungi

Mwenyekiti wa chama cha UDP, John Cheyo amesema kutokana na changamoto ya muda kuwa mfupi itakuwa ngumu kwao kujirekebisha.

“Lakini sheria imetungwa mwaka huu, tuna uchaguzi mwaka huu, na uhakiki mwaka huu tutajirekebisha kwa muda gani” amesema Cheyo.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema anafahamu uwepo wa sheria na kuomba kipindi cha miezi mitatu kwenda kujipanga kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo.

Naye Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chadema, Benson Kigaila amesema orodha ya wanachama wa chama cha siasa ni sawa na usajili wa wapiga kura na wanachama wanakuwa hai kama wanatembelewa.

Naibu Katibu Mkuu  wa CCM, Abdallah Juma Saadala amesema anaunga mkono mchakato huo  uendelee huku Mwenyekiti wa Chauma, Hashim Rungwe akiwataka wanachama kukaa tayari kwa uhakiki huo.

Uhakiki huo umekuwa ukifanyika kila mwaka kasoro mwaka 2019 na 2018 kutokana na mchakato wa kuandaa sheria ya vyama vya siasa na watakutana baada ya Aprili 20, 2020 kufanya majumuisho.