Ujasiri ni muhimu katika kumkomboa mwanamke

Dar es Salaam. Wanawake nchini wameshauriwa kuwa na ujasiri katika kutafuta na kulinda haki zao katika familia kama nyenzo muhimu ya kuwaepusha na athari za kuangukia katika umaskini.
Hayo yamesemwa na Orester Komba kutoka wilaya ya Mbinga, Mkoani Ruvuma wakati akitoa maelezo ya ushuhuda wa namna alivyoweza kupambana kudai haki yake pale ambapo aliyekuwa mumewe alitaka kumnyang’anya baada ya kutokea mtafaruku kati yao.
“Nawashauri wanawake wenzangu nchini ambao wanapitia katika changamoto za kunyimwa haki katika familia kuwa jasiri na kuomba ushauri wa kisheria ili kuweza kupata haki yao na kuwawezesha kuishi Maisha mazuri,” alisema.
Orester Komba ni mama wa Watoto wawili na mke wa Kelvin Milinga aliingia kwenye mgogoro baada ya aliyekuwa mumewe kuuza nyumba waliyojenga pamoja bila kumshirikisha.
Kufuatia hatua hii, Orester alisaidiwa na wasaidizi wa kisheria wa kituo cha NAJATA kinachofanya kazi wilayani Mbinga na kurudishiwa kiasi cha fedha ambazo alizitumia kujenga nyumba nyingine anayoishi sasa.
NAJATA ni shirika la wasaidizi wa kisheria chini ya ufadhili wa Legal Services Facility ambao wanafanya kazi nchi nzima, Tanzania Bara na visiwani Zanzibar na wasaidizi wa kisheria zaidi ya 3900. Kwa wastani kwa mwaka wasaidizi wa kisheria ushughulikia takribani zaidi ya kesi 70,000 ambapo asilimia 60 ya kesi hizi wanazitatua wakati asilimia 22 zinakuwa bado zinaendelea, asilimia 16 zimepelekwa kwa vyombo vya juu kwa utatuzi huku asilimia 2 ya kesi zinazowafikia zikishindwa kupatikana usuluhishi.  Kesi zinazotatuliwa kwa wingi na paralegal ni pamoja na kesi za ardhi, ndoa, matunzo kwa watoto, jinai, na ukatili wa kijinsia.
Msaidizi wa kisheria kutoka NAJATA, Samuel Kayuni ndiye alichukua jukumu la kumsaidia Orester kutafuta suluhisho la mgogoro huo na ili kufanya hivyo alilazimika kuzikutanisha familia mbili za wanandoa hao kwa kusudi la kumsaidia mwanamke huyo apate mgao wa fedha na mali walizochuma pamoja.
''Hata hivyo juhudi zangu hazikufanikiwa kwa sababu Kelvin na ndugu zake walidai kwamba mwanamke hana haki ya kupata mgao wa fedha wala mali, hata mwanaume akifariki hana haki ya kurithi chochote'', alisema Kayuni.
Msaidizi huyo wa kisheria alisema kutokana na kutoridhishwa na majibu hayo alimshauri Orester  akafungue kesi ya madai  mahakamani, ushauri ambao uliridhiwa na Orester na ndugu zake.
Baada ya mwaka mmoja mahakama ilimpa ushindi na kumuamuru Kelvin ampe nusu ya fedha za mauzo ya nyumba kiasi cha Sh 15milioni kisha vyombo na samani viwagawanywe kwa usawa.
 “Nawasihi wanawake wenzangu ambao wapo kwenye matatizo kama niliyopitia mimi wajifunze nilichofanya mimi na watafute msaada katika mashirika ya utetezi wa haki za binadamu na vituo vya msaada wa kisheria vilivyopo katika wilaya wanazoishi. Maisha yangu yamepitia changamoto nyingi sana lakini leo yako kwenye mwanga na ninafurahi kuona hatua ambayo nimepiga”, anamalizia Orester.
Orester sasa anafanya biashara ya kuuza chakula katika Shule ya Sekondari ya Mbinga, kazi inayompa uwezo wa kuishi vizuri kuliko awali huku akikusudia kukuza mtaji wake ili atanue biashara yake zaidi.