Breaking News

MUUNGANO TANGANYIKA-ZANZIBAR 1964: Ujerumani Magharibi, Mashariki zatishia uhai wa Muungano-16

Thursday April 25 2019

Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere

Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere akisalimiana na Abdulrahman Babu 

Balozi wa Marekani nchini Tanganyika aliendelea kufanya mawasiliano na nchi yake kuhusu mambo yanavyoendelea na mapendekezo yake ya nini kifanyike. Alitaka Rais Julius Nyerere apewe msaada wowote ambao angehitaji.

Lakini pia alilisisitiza jambo moja; alisema iIi kuwe na matokeo mazuri, ni lazima kuwe na “uthibitisho kwamba dunia itawajibika kikamilifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika-Zanzibar kwa kutoa misaada kwa maendeleo ya Zanzibar inayofikia pauni milioni mbili ili kugharamia miradi iliyokubaliwa”.

“Michango kutoka kwa wahisani wengine, hasa Uingereza na Jamhuri ya Ujerumani ni muhimu, yote ikiwa ni kwa kutoa misaada ya kifedha na kuepuka muonekano wowote utakaoonyesha kwamba Marekani inataka kufanya mapinduzi, lakini kama mashauri ya dharura yataonekana kuwa hayafai, naamini kwamba Marekani itatoa uthibitisho na hata msaada wa hisani baadaye,” aliandika.

Lakini kama Marekani na Uingereza walidhani kuwa Abdulrahman Babu na kundi lake ndio walikuwa tatizo pekee la Zanzibar kutokana na imani yao katika ukomunisti huko Zanzibar, hawakuwa sahihi. Maelezo yaliyofuatia baada ya Marekani na Uingereza kutaka kuhakikisha kwamba Babu na kundi lake hawana chao Zanzibar, yalionyesha kwamba kulikuwa na matatizo mengine pia. Kuliibuka mgogoro kati ya Tanganyika na Zanzibar kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani (GDR).

Zanzibar iliitambua serikali hiyo na kuipa utambulisho wote wa kibalozi. Na hiyo ni nchi pekee iliyoweza kufanya hivyo nje ya kambi ya nchi za kijamaa. Tanganyika haikuwahi—na pengine haikuwa tayari—kuitambua serikali ya nchi hiyo, badala yake, Tanganyika ilikuwa na uhusiano mzuri sana na Ujerumani Magharibi (FRG).

Haikuwa rahisi—au labda haingewezekana—kwa nchi yoyote duniani kuwa na uhusiano wa kibalozi na Ujerumani Magharibi na wakati huohuo ikawa na uhusiano kama huo na Ujerumani Mashariki. Kuwa na uhusiano wa kibalozi na Ujerumani moja ni sifa ya kupoteza uhusiano wa aina hiyo na Ujerumani nyingine.

Advertisement

Serikali hii ya mwisho ilikuwa na kile kilichojulikana kama ‘Holstein Doctrine’ ambacho kiliweka masharti kwamba nchi yoyote iliyoitambua na kuwa na uhusiano wa kibalozi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani (GDR), moja kwa moja ingepoteza uhusiano wake na serikali ya Jamhuri ya Ujerumani (FRG).

Tanganyika isingeitambua Ujerumani Mashariki kwa sababu ya mkataba wake na Ujerumani Magharibi. Lakini Zanzibar haikuwa na tatizo hilo kwa sababu Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani haikuweka masharti yoyote ya kutambuliwa kwake.

Jumatatu ya Mei 4, 1964 kulikuwa na mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Serikali ya Muungano ambako suala la Ujerumani lilijadiliwa. Kama ilivyotazamiwa na wataalamu wengi wa mambo ya siasa, kikao hicho cha mawaziri kiliisha kwa mvutano mkubwa.

Hali hii ilizuia maendeleo ya hatua nyingine za masuala ya Muungano na hivyo kusababisha maofisa wa serikali za Uingereza na Marekani waliokuwa katika miji ya Zanzibar na Dar es Salaam kuwa katika hali tete.

Kile walichokipigania kisirisiri na katika kipindi cha karibu siku 100 na kuonekana kana kwamba kimefanikiwa, sasa kilikuwa katika hatari ya kuvurugika.

Mawaziri walioteuliwa na Nyerere Aprili 27, siku saba tu baadaye walifanya kikao chao kilichomalizika bila maelewano. Kulikuwa na hoja nyingi zilizobishaniwa kuhusu suala la Ujerumani. Wakati walipoanza kufikiri kwamba kazi yao ya kuhakikisha kwamba nchi hizo zinaungana imekwisha, ndipo wakagundua kwamba kazi waliyoifanya ilikuwa ndogo kuliko ile ambayo ilikuwa haijafanyika.

Hawakutambua kuwa kulikuwa na mambo mengi sana ambayo hawakujua na walipotambua hilo walipata wasiwasi zaidi.

Kwa kuwa kutengana ni rahisi zaidi kuliko kuungana, walitambua kwamba ingawa jitihada za kuziunganisha nchi mbili zilihitaji kazi na nguvu kubwa, lakini jitihada za kuhakikisha Zanzibar na Tanganyika zinaungana zilikuwa kubwa zaidi. Balozi mdogo wa Marekani visiwani, Frank Carlucci alitaarifu kwamba bado kulikuwa na Wakomunisti Zanzibar na kwamba walikuwa wakiipinga waziwazi Serikali ya Muungano.

“Ni jambo la wazi kabisa kwamba kuanzia juu (pengine akimaanisha kuanzia ngazi za juu za utawala) na kutokana na mjadala mkali unaoitia homa unaoendelea kuhusiana na shughuli za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani, mashambulizi makubwa yanahitajika,” aliandika. “Nina mashaka sawasawa na Balozi (William) Leonhart kwamba mwonekano wowote wa kukokota miguu (pengine akimaanisha kulegalega) kutakuwa jambo hatari sana kwa juhudi za Nyerere za kuvunja himaya ya ukomunisti Zanzibar..”

Jumamosi ya Mei 9, Carlucci alikwenda kwa katibu mkuu wa chama cha Afro-Shiraz, Sheikh Thabit Kombo na kuzungumza naye kuhusu Muungano.

Carlucci alipanga mazungumzo yao yafanyike mchana. Hakuwa amempa taarifa mapema, lakini Thabiti alimkaribisha.

Carlucci anaelezewa katika kitabu cha “Carlucci Versus Kissinger” kilichoandikwa kwa pamoja na Bernardino Gomes na Tiago Moreira de Sa, kuwa ni muanzishaji mada, msikilizaji na mdadisi, stadi alizotumia pia katika mazungumzo yake na Kombo.

Baada ya kupata maoni na msimamo wa Kombo, Carlucci alimwambia anavyofahamu jinsi Kombo na Abeid Karume wanavyoupenda Muungano na kumjulisha kuwa Marekani itawaunga mkono na kuwapa msaada wanaohitaji.

Kwa kuwa muda wote wa mazungumzo hakumkatiza Kombo hata mara moja, Carlucci alimfanya Sheikh Kombo ajione kuwa ni mtu wa maana sana. Na kila alichohitaji kilikubaliwa na Carlucci. Uzoefu wake katika ujasusi ulimsaidia sana kumshawishi mtu aliyekutana naye.

Katika mazungumzo yao, Carlucci alisema: “Kama hili (la kuvunjika kwa Muungano) litatokea, Wakomunisti na (Abdulrahman) Babu watafanikiwa na Karume na Zanzibar watapata hasara kubwa.

“Karume ameonyesha mfano wa kuigwa kwa umoja wa Afrika na hatuwezi kuuharibu mfano huu kwa sababu ya suala la vita baridi ambalo Zanzibar ilikuwa imeshapotea tofauti na nchi nyingine za Afrika.”

Kisha Carlucci akamhakikishia Thabiti kwamba Ujerumani Magharibi imejiandaa “kuchukua miradi yote” ya Ujerumani Mashariki na kwamba “Zanzibar itapoteza mambo mengi lakini “haitapata chochote kwa kung’ang’ania kuitambua na kuendeleza uhusiano wa kibalozi” na Ujerumani Mashariki.

Itaendelea kesho

Advertisement