Breaking News

MUUNGANO TANGANYIKA - ZANZIBAR 1964: Ujerumani Magharibi wamkera Nyerere awajia juu- 17

Friday April 26 2019

 

By William Shao

Mijadala kuhusu uhai wa Muungano uliokuwa mchanga wakati huo ilizidi kuenea sehemu nyingi, huku waumini wa ukomunisti wakionekana kuwa hatari kwa Zanzibar na Muungano kwa ujumla.

Baadhi ya waandishi na wachambuzi wa mambo waliofuatilia hali ya kisiasa ya Zanzibar katika kile kipindi cha miezi mitatu muhimu ya mwanzo, walikuwa na wasiwasi kwamba Zanzibar ilikuwa haijakombolewa kikamilifu na kuingizwa katika familia ya Afrika Mashariki au Afrika.

Oscar Kambona ni mmoja wa watu walioamini hivyo, lakini ambao hawakutaka kuzungumza waziwazi maono yao.

Lakini tofauti na wengine, Kambona alikuwa na jukwaa la kusemea kama angetaka kufanya hivyo.

Wakati fulani, Kambona alikaririwa na chombo kimoja cha habari akisema “Zanzibar haijatokomea”.

Lakini aliona ukombozi wa kweli ni uchumi imara.

Advertisement

“Kwa kweli tunahitaji uchumi imara na sera nzuri. Ugumu kwetu sisi si kule kuchagua kati ya Mashariki na Magharibi. Ugumu wetu upo katika kuchagua kati ya ukomunisti wa kimataifa na ujamaa wa Kiafrika,” alisema.

“Sasa Karume ni Mwafrika, Kassim Hanga ni Mkomunisti, lakini ni Mwafrika pia. Namjua hasa, tena namjua sana. Ni rafiki yangu sana. Tukiwa na watu hawa wawili (Karume na Hanga) inawezekana Zanzibar haijakombolewa kwa ajili ya Afrika na Waafrika.”

Wakati hayo yakiendelea, tangu pale mwanzoni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulimaanisha jambo moja kubwa kwa Zanzibar—kwamba haiwezi kuwa na dola lake yenyewe.

Pia kulikuwa na matatizo mengi yaliyoukabili Muungano wa Tanzania. Urusi na Marekani walielekea kuifanya Zanzibar kuwa mojawapo ya viwanja vyao vya kuendeshea siasa zao barani Afrika.

Kama ambavyo Marekani waliishinikiza Zanzibar kuungana na Tanganyika, Warusi nao walikuwa na mbinu nyingine.

Gazeti la The Times la Uingereza (Mei 27, 1980), ikiwa ni miaka 16 baada ya Muungano, liliwahoji baadhi ya wanasiasa kuhusu mambo katika miaka ya 1960 yalivyokuwa yakifanyika.

Gazeti hilo lilimhoji ofisa wa Shirika la Kijasusi la Urusi (KGB), Igor Kocl Ilya Dzhirkvelo ambaye alikuwa Afrika Mashariki wakati wa Mapinduzi na hatimaye Muungano.

“Mbinu za Kirusi katika Bara la Afrika zilishindwa, sana sana hiyo ni kutokana na serikali ya Moscow kutotambua hali za Kiafrika. Zilitumika zaidi dawa za Kirusi kutibu magonjwa ya siasa za Kiafrika badala ya kutumia dawa za Kiafrika kutibu magonjwa ya siasa za Kiafrika,” alisema Dzhirkvelov.

Mara baada ya Muungano, Serikali iliugeuza ubalozi wa Ujerumani Mashariki mjini Zanzibar uonekane kama ofisi za biashara ya kimataifa tu, lakini Karume aliligomea jambo hilo, na akaitaka Serikali ya Muungano iitambue Ujerumani Mashariki na kuachana na Ujerumani Magharibi.

Kwa kusikia kauli ya Karume, Ujerumani Mashariki ilizidi kumimina misaada kwa serikali ya Karume na hata viongozi wakubwa wa kisiasa wa nchi hiyo waliitembelea Zanzibar. Haya yalikuwa kati ya matukio yaliyoumiza kichwa cha Mwalimu Nyerere.

Katika siku za mwisho za maisha yake, Nyerere alionekana kuwa aliweka moyoni kadhia hizo.

Akijibu maswali ya waandishi kuhusu matukio ya miaka ya 1960 yaliyohusisha Ujerumani Magharibi, Mashariki, Zanzibar na Tanganyika, Nyerere alitema nyongo.

“Ilinifedhehesha sana. Nachukia sana kutishwa. Kwa nini Wajerumani waone kuwa uhusiano wao na watu wengine ni wa maana zaidi kuliko uhusiano wa Watanzania na watu wengine?” alihoji Nyerere.

Wakati huo, Sheikh Karume alikuwa na msimamo mkali kuhusu uhusiano wa Zanzibar na Ujerumani Mashariki, hivyo Ujerumani Magharibi ilikuwa inamshinikiza Nyerere abadili mwelekeo na kuachana na wajamaa hao wa Kijerumani.

Nao Ujerumani Mashariki walimjia Karume na wazo lenye uzito mbaya zaidi kwa heshima ya Nyerere. Walimpa Karume masharti kwamba ili waendelee kumsaidia na ili aache kuburuzwa na Nyerere, njia bora zaidi ni kuvunja Muungano wa Tanzania. Hili lilikuwa jambo la mwisho ambalo Nyerere angefanya ikiwa ilikuwa ni lazima kulifanya.

Hii haikuwa fedheha kwa Nyerere tu, bali hata kwa wale walioshiriki katika harakati za kuhakikisha kwamba Tanganyika na Zanzibar zinaungana kwa gharama zozote.

Nyerere alianza kuwa mwangalifu zaidi. Tanzania ikawakubali wajumbe wawili wa Ujerumani Mashariki ili kuunusuru Muungano wa Tanganyika-Zanzibar na katikati ya mwaka 1964, Nyerere alitoa nafasi moja ya balozi wa Taifa hilo aje kuishi Dar es Salaam au Zanzibar.

Jambo hili lilipingwa na Ujerumani Mashariki yenyewe, ambayo msaidizi wa Waziri Mkuu wake, Kiesewetter, alizuru Zanzibar mapema 1965 kushinikiza jambo hilo. Kwa mara nyingine Nyerere alilazimika kuwakubali wajumbe wawili wa Ujerumani Mashariki kuja Tanzania—mmoja awe Zanzibar na mwingine abaki Dar es Salaam, hatua hiyo ikaifanya Ujerumani Magharibi ihisi kusalitiwa.

Nyerere alipoona kuwa hatua hiyo inaharibu uhusiano wake na Ujerumani Magharibi, aliwaita wajumbe na maofisa wengine wa Taifa hilo na kukutana nao Ikulu mjini Dar es Salaam, na baada ya chakula cha jioni, aliwaambia kuwa tatizo hilo lingezungumzwa na lingemalizika. Wajumbe wa Ujerumani Magharibi walikataa hoja hiyo.

Ujerumani Magharibi iliwaondoa wanajeshi wake waliokuwa wakiwasaidia wanajeshi wa Tanzania. Walikwenda hata mbali zaidi ya hapo.

Pamoja na kuwaondoa maofisa wake wa kijeshi, waliondoa misaada ya kijeshi kwa Tanzania kisha wakatishia kusimamisha misaada yote. Siku moja katikati ya mwaka 1965, Rais Nyerere alituma ujumbe kwenda kwa balozi wa Ujerumani Magharibi mjini Dar es Salaam, Dk Herbert Schroeder.

“Kwa ajili ya uamuzi wa Serikali yako wa kuondoa wataalamu wa mambo ya kijeshi waliokuwa wanafundisha wanajeshi wetu hapa nchini chini ya mpango wa Ujerumani wa kutoa msaada, sasa ningependa Ujerumani iache kutoa msaada wowote kwa Tanzania. Ujerumani ikomeshe misaada sasa.” Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Magharibi, George Kahama, ambaye wakati wa sakata hilo alikuwa mjini Dar es Salaam aliwaambia waandishi wa habari kuwa alipokuwa huko Ujerumani Magharibi aliwaambia wakuu wa serikali hiyo kuwa ikiwa watakomesha misaada mingine kwa Tanzania, “Ujerumani Magharibi ndiyo itakayoumia, si Tanzania”.

Kahama, aliyewasili mjini Dar es Salaam siku moja kabla ya kutoa taarifa hiyo, alizungumza na Mwalimu Nyerere kwa muda wa saa tatu mfululizo.

Pamoja na kwamba wakati fulani mambo yalionekana kutulia, kwa muda fulani hakuna misaada iliyoendelea kutolewa na Ujerumani Magharibi kwa Tanzania. Hili ndilo lililomkera sana Mwalimu Nyerere kiasi cha kutoa ile kauli kwamba “nachukia kutishwa”.

Advertisement