Ujumbe wa Freeman Mbowe kwa KKKT, Askofu Shoo

Saturday August 24 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe ametoa salamu za pongezi kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa kumaliza mkutano mkuu salama na kupata Mkuu wa Kanisa hilo atakayeongoza kwa kipindi cha miaka minne.

Katika mkutano huo wa 20 uliomalizika usiku wa kumakia leo Jumamosi Agosti 24, 2019 ambapo Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Fredrick Shoo alitangazwa na Mwenyekiti wa uchaguzi, Blaston Gavile kuwa Mkuu wa Kanisa hilo kuendelea na nafasi hiyo kwa miaka minne mingine.

Katika salama za Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini humo alizozitoa leo Jumamosi ameanza kwa kusema, “Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuwaongoza, kuwasimamia hata kuwajaza busara na subira hadi kufikia kwa pamoja na kwa umoja wenu kupata Mkuu wa Kanisa atakayeongoza Kanisa la Bwana kwa miaka minne ijayo.”

Mbowe anasema Taasisi zetu za Kiroho (Waislamu na Wakristo; wa madhehebu mbalimbali na hata Makundi mengine ya Imani tofauti) zimejipambanua kuwa nguzo muhimu ya kujenga amani na upendo kwa kila mmoja na hatimaye umoja katika familia/kaya na mwishoni Taifa kwa ujumla wake.

 

“Hata hivyo, ni busara zaidi kwa taasisi zetu kutambua wakati wote kuwa amani, upendo na umoja wa kudumu unajengwa kwenye msingi wa haki na kweli,” amesema Mbowe

Advertisement

“Ni chini ya dari zao, makundi na hata viongozi mbalimbali wenye mitazamo tofauti wamekutana na kufanya toba na hata upatanisho tena kwa unyenyekevu mkubwa! Wajibu huu ni endelevu na unastahili kuenziwa bila kuchoka wala kuogopa,” ameongeza

Mbunge huyo wa Hai amesema, “Taasisi za dini zilizo imara kiroho, kijamii na hata kiuchumi ni kiunganishi muhimu cha Taifa na sisi kama Watanzania tuna wajibu muhimu kuombea amani na upendo uliosimama juu ya haki na kweli katika kujenga umoja miongoni mwetu.”

Amesema mifarakano ya asili au ya kutengenezwa ndani ya Taasisi zetu za dini, Kisiasa na hata Kijamii haiwezi kuiacha nchi yetu salama. Tunaomba mkono wa Mungu wetu ukalitunze jambo hili na kuzima nguvu zozote za shetani. Akaruhusu kweli na haki kutamalaki popote na Watanzania wote wakaishi maisha ya furaha na yenye matumaini chanya.

“Kwa Uongozi mpya wa KKKT, tunawaombea uwezo wa Mwenyenzi Mungu katika kuutenda wajibu wenu wa kuliimarisha Kanisa na jamii yote iipendayo na kuiamini haki. Bwana wetu Yesu Kristo apewe sifa sana,” amemaliza Mbowe katika salamu zake

Advertisement