Ujumbe wa Maalim Seif kwa Magufuli

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo ya faragha na Mwanasiasa Mkongwe ambaye ni Mwanachama wa Chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya kukutana kwa faragha, mwanasiasa maarufu nchini, Maalim Seif Shariff Hamad amemshauri Rais John Magufuli kukutana na viongozi wote wa vyama vya upinzani kujadili kwa pamoja uchaguzi mkuu, hususan uhuru wa chombo cha kusimamia kazi hiyo.
Maalim Seif amesema hatua hiyo itawezesha pande zote kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu kile wanachokizungumza kuhusu maandalizi ya mazingira ya uchaguzi na kuuwezesha kuwa wa amani, huru na wa haki.
Maalim Seif alitoa ushauri huo jana alipozungumza katika mahojiano maalum na wahariri wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata relini Dar es Salaam, siku moja tangu Rais Magufuli akutane kwa nyakati tofauti na viongozi watatu wa upinzani Ikulu.
MCL ni wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti pamoja na MCL Digital, ambayo ilirusha moja kwa moja mahojiano hayo katika chaneli yake ya Youtube kwa saa 1:31.
Mbali na Maalim Seif, wengine waliokutana na Rais ni mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba na wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Maalim Seif alidokeza kuwa yeye ndiye aliyeomba kukutana na Rais na kwamba aliandika barua mara tatu bila ya majibu kabla ya kuitwa juzi asubuhi na katibu wa Rais na kupewa wito huo.
Pia alidokeza alichozungumza na mkuu huyo wa nchi, akisema ni kuhusu matatizo ya Zanzibar, tofauti na juzi aliposema mazungumzo yao yalijikita katika masuala mbalimbali yakiwamo uchaguzi mkuu na haja ya kudumisha amani, usalama na upendo.
Alipoulizwa kama Rais ataendelea kukutana na viongozi wengine tofauti na hao watatu ambao alishakutana nao awali, mkuu wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa alisema suala hilo ni siri ya ratiba za Rais.

Ushauri wa Maalim Seif
Maalim Seif, aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, alisema licha ya mazungumzo ya juzi bado anaona mahitaji ya kuwapo kwa mazungumzo yatakayowahusisha wapinzani wote na si mmoja mmoja.
“Nafikiri Rais anatakiwa akutane na vyama vya upinzani na wajadili suala la tume huru,” alisema Maalim Seif, ambaye pia aliwahi kuwa waziri kiongozi.
“Patakuwa na hoja za upande wao (Serikali) na wapinzani nao wana hoja zao. Majibu yatakayotolewa yatafika mahali mtasikiliza na kuridhika.
“Rais aitishe kikao cha viongozi wa vyama kwa pamoja na baada ya hapo mnaweza kuzungumza mnaendeleaje. Hatua ya kwanza angekutana na vyama”.
Maalim Seif alisema walipokutana na Rais Magufuli Novemba 12 mwaka jana jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa kitabu cha Rais Benjamin Mkapa cha “My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusudi Langu) alimuomba miadi ya kukutana naye.
“Kwa hiyo dhamira yangu ilikuwa nikutane na Rais kwa sababu yeye si Rais wa Tanganyika, ni Rais wa Tanzania. Yanayotokea popote Tanzania yanamhusu. Kwa hiyo mazungumzo yangu yalijikita katika hali hiyo ya Zanzibar na kweli nilizungumza yote niliyokuwa nayo moyoni,” alisema.
Alipoulizwa na mmoja wa wahariri iwapo ana matumaini kiasi gani ya kutekelezwa kwa yale waliyoteta na rais, Maalim Seif alisema: “Siwezi kusema asilimia 100 kuwapa uhakika wa kikao cha jana (juzi), kwa sababu haya mamlaka na madaraka hayapo mikononi mwangu, yapo kwa Rais Magufuli mwenyewe.”
Alisema kwa wakati alipokutana naye mara ya kwanza, hangeweza kujibu mambo yote aliyomwambia kwa kuwa ndio kwanza alikuwa anaingia madarakani.
Alisema hivi sasa ameshakaa madarakani kwa zaidi ya miaka minne, anaweza kuyafanyia kazi kwa kuwa anafahamu yanayoendelea Zanzibar, ambako alisema hali ni mbaya.
Alisema Zanzibar kuna matatizo mengi na baadhi yake ni ya kihistoria na kwamba yaliwahi kufika mahali watu wakaacha kusalimiana na hata ndugu kutozikana.

Tume huru ya uchaguzi
Maalim Seif pia alizungumzia ahadi ya Rais kwamba uchaguzi mkuu ujao utakuwa huru na wa haki, akisema majadiliano hayo na Rais, lazima yaguse tume huru ya uchaguzi na muundo wake.
“Tuzungumze jinsi ya kupatikana kwa mwenyekiti, mkurugenzi na sekretarieti nzima ili kuwa tofauti na ilivyo sasa kwa kuwa wanateuliwa na Rais ambaye ni mwenyekiti wa CCM na wakati mwingine yeye mwenyewe anakuwa mgombea,” alisema Maalim Seif.
“Nadhani hilo Rais angelifanya. Wakurugenzi (wa uchaguzi) ni sehemu ya sekretarieti ya tume na wote wale ni makada wa CCM. Na hawa wameshaambiwa kwamba lazima waiangalie CCM maana ndio imewafikisha hapo walipo.”
Katibu mkuu huyo wa zamani wa CUF alisema katika mazingira hayo “itakuwa jambo la ajabu kuwatangaza wapinzani. Nchi hii watu wengi wanategemea riziki kutoka serikalini. Wapo wanaojiajiri wenyewe ila wa serikalini kila mmoja ana hofu asipoteze kitumbua chake.”
Alisema mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba ni mazuri yanataka kufanana na ya nchini Kenya ambako ajira za watumishi wa tume hutangazwa na waombaji hupitia katika mchakato na hatimaye wanaokidhi vigezo majina hupelekwa kwa Rais ambaye kazi yake huwa ni kutangaza tu.
Alipoulizwa kama muda unatosha kufanya mabadiliko hayo ya tume ya uchaguzi, Maalim Seif alisema: “sasa hivi wakati umefika. Inawezekana, hakuna kisichowezekana.
“Zanzibar tulipotaka maridhiano muda ulikuwa mfupi, lakini iliwezekana. Mapendekezo ya tume ya Jaji Warioba yapo pale na yanasema nini kuhusu tume huru, kwanza fanyeni hayo.
“Zanzibar tungekuwa na watu waadilifu ingekuwa nafuu. Tume (ya uchaguzi Zanzibar -ZEC) inaajiri yenyewe kuanzia wilaya hadi majimbo, ila kutangaza matokeo ni kujaribu kuonyesha sheria imefuatwa ila wanaoteuliwa ni wa mrengo wa huko. ZEC wangetafuta watu wanaoaminika ingekuwa nafuu kuliko Bara”.
Rasimu ya Katiba iliweka masharti ya upatikanaji wa wajumbe wa tume ya uchaguzi kwa uwazi kupitia utaratibu wa kuomba nafasi na kuchujwa na kamati ya uteuzi kabla ya kuteuliwa rasmi na Rais kisha kuthibitishwa na Bunge.
Katika rasimu hiyo ilipendekeza kamati ya uteuzi wa mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wa Tume kwamba iundwe na Jaji Mkuu wa Tanzania (mwenyekiti), maspika wa Bunge la Tanzania, wa Tanganyika na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Wajumbe wengine ni Jaji Mkuu wa Tanganyika, Jaji Mkuu wa Zanzibar na mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi na Uwajibikaji.

Katiba mpya
Kuhusu mchakato wa katiba, Maalim Seif alisema unapaswa kuendelea kwa kuanzia pale Tume iliyoongozwa na Jaji Warioba ilipoishia kwani nyaraka na taarifa mbalimbali iliyokusanya kutoka kwa wananchi zipo.
Mwanasiasa huyo mkongwe nchini, alitofautiana na kile alichokisema Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alioufananisha na kiporo cha chakula ambacho “kimechacha na hakiwezi kulika tena”.
Jumanne iliyopita akizungumza na wahariri wa MCL, Dk Bashiru licha ya kutaka wananchi waachwe wazunguze kuhusu katiba wanayoitaka lakini alisema ili kiporo hicho kisije kuwaumiza matumbo watakaokula, kinapaswa kuandaliwa chakula kizuri chenye afya na lishe.
Hata hivyo, Maalim Seif alisema alifurahishwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete alipouanzisha mchakato huo lakini alionyesha kusikitishwa na ulipoishia hasa Bunge Maalum la Katiba ilipobadili mambo mengi yaliyokuwamo kwenye Rasimu ya Jaji Warioba.
Mchakato huo uliishia kwa kupata Katiba inayopendekezwa na hatua iliyokuwa inafuata ni kufanyika kwa kura ya maoni Aprili 30, 2015 lakini haikufanyika kutokana na kutokamilika kwa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Februari 10, Jaji Warioba alisema anaamini kuwapo kwa matamanio ya wananchi juu ya kutimizwa jambo hilo kwa kutumia Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013 na Sheria ya Kura ya Maoni ili kuuhitimisha mchakato huo.