VIDEO: Ulega: Hatujafunga masoko ya samaki, mifugo Tanzania

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi , Abdallah Ulega akizungumza na wafanyabiashara wa soko la samaki la Feri.

Muktasari:

Serikali ya Tanzania yawatoa hofu wafanyabiashara wa masoko ya samaki na mifugo kwa kuwaeleza masoko yao hayatafungwa, yawataka  kuindelea kuchapa kazi kwa kuchukua tahadhari zote zilizoshauriwa na wataalam  wa afya namna ya kujikinga na corona

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania, Abdallah Ulega amewatoa hofu wafanyabiashara wa masoko ya samaki na mifugo, akisema masoko hayo hayatafungwa kama inavyosemwa kutokana na virusi vya corona.

Ulega ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Machi 28, 2020 wakati alipozungumza kwa nyakati tofauti na wafanyabiashara wa soko la samaki la Feri na mnada wa mifugo wa Pugu wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.

“Endeleeni na biashara ila chukueni tahadhari, tumeweka utaratibu kila mtu anayeingia na kutoka sokoni ahakikishe ananawa mikono yake na sabuni kama ilivyoshauriwa na wataalamu wa afya.”

“Naomba niwatoe hofu maana nasikia kuna masoko yetu mengine wilayani huko yameanza kufungwa. Nawaelekeza wakurugenzi wote nchini wasifunge masoko ya mifugo na samaki bila kuitaarifu wizara,” amesisitiza  Ulega.

Katika maelezo yake, Ulega amepata taarifa kuwa hivi sasa  kuna shida ya  namna ya ng’ombe kutoka mikoani kwenda mnada wa Pugu kwa sababu kuna watu wameenza kuzuia minada.

“Serikali haijatoa maelekezo ya kuzuia minada, tunataka biashara iendelee. Maelekezo ya Serikali biashara iendelee, isipokuwa wafanyabiashara na wafugaji wachukue tahadhari dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona,” amesema Ulega.

Amewataka wafanyabiashara hao kuzingatia tahadhari za kujikinga na virusi hivyo, katika utekelezaji wa majukumu yao, akisema wakati huu dunia inahangaika na corona lazima wafanyabiashara wa samaki na mifugo wajiongeza kupata fikra mpya.

Mfanyabiashara wa mifugo wa mnada wa Pugu, Nickas Makenze ameshukuru Ulega kwa kuwatoa hofu kuhusu maneno yaliyokuwa yakisambaa kuwa huenda masoko hayo yakafungwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa virusi vya corona.

“Tulishaanza kupata taarifa kuwa mikoani minada inafungwa, sasa tulikuwa tunawaza tutafanyaje wakati biashara hii tunaitegemea. Tulishaanza kupata misukosuko na tulizieleza familia zetu kuwa muda wowote mnada utafungwa,” amesema Makenze.

Awali, mkurugenzi wa manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri amesema wafanyabiashara wa soko la Feri wanaendelea na shughuli zao kama kawaida huku manispaa hiyo ikichukua tahadhari za kuwahakikisha wanajikinga na virusi vya corona katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Tuna uhakika biashara itakwenda vizuri ingawa hivi sasa kuna changamoto ya kushuka kwa soko la samaki aina ya dagaa kamba kwa sababu watalii wengi hawaji kwenye hoteli kubwa,” amesema Shauri.