Ulega alivyotatua kero ya wananchi kwa kumpigia simu bosi TFS

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdalla Ulega akifurahi na wananchi wa kijiji cha Kwengoma kata ya Kwamatuku wilayani Handeni,baada ya kuwaahidi kupelekewa boti kwaajili ya shughuli za uvuvi katika eneo hilo leo. Picha na Rajabu Athumani.

Muktasari:

Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania, Abdalla Ulega amefanya ziara wilayani Handeni Mkoa wa Tanga na kukutana na malalamiko kutoka kwa wananchi wanaoishi karibu na Hifadhi ya Msitu wa Mtungulu ambapo ametumia simu yake ya kiganjani kumwelekeza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo kwenda kumaliza suala hilo.

Handeni. Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania, Abdalla Ulega amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo kutatua sitofahamu iliyopo katika Hifadhi ya Msitu wa Mtungulu wilayani Handeni Mkoa wa Tanga.

Ulega amesema eneo hilo limekuwa kero kutokana na kutokuwa na alama za kuonyesha mipaka ya hifadhi hivyo na kuleta kero kwa wananchi.

Naibu waziri huyo alitoa maagizo hayo baada ya kupokea kero za wananchi leo Jumamosi Februari 22,2020 katika soko la Ndelema kwenye ziara yake ya siku moja.

Amesema siyo sawa kwamba mwananchi atozwe faini kwa kosa la kuingiza mifugo katika hifadhi huku kukiwa hakuna alama yoyote.

Kutokana na  hali hiyo, Ulega ilimlazimu kumpigia simu Profes Silayo na kumtaka kutatua kero hiyo haraka kwani siyo sawa kwa watendaji wake wanachokifanya kwa wananchi wa Magamba wanaoishi karibu na hifadhi hiyo ya Mtugulu.

Profesa Silayo akijibu kero hiyo alisema atatuma timu Jumatatu ya Februari 24,2020 katika msitu huo wa hifadhi kwenda kutatua kero husika.

Amemhakikishia Ulega suala hilo litafanyiwa kazi haraka ili kero inayowapata wananchi wa Magamba iweze kupata majawabu na kuepukana na faini wanazotozwa kwa kuingia kwenye hifadhi husika.

Awali, Bali Njoe mkazi wa Magamba alisema katika eneo hilo wananchi wanatozwa faini mara kwa mara kwa mifugo yao kuchukuliwa na watu wa Serikali wakidai mifugo inaingia kwenye hifadhi huku kukiwa hakuna mpaka wowote.

Alimuomba naibu waziri huyo kufanyia kazi changamoto husika kwa wakati kwani wahusika wanaolinda msitu huo wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi.