Umasikini chanzo cha maambukizi mapya ya Ukimwi

Wednesday September 11 2019

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Umasikini umetajwa kuwa moja ya changamoto inayochangia wasichana wadogo kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi baada ya kuamua kujiingiza katika shughuli hatarishi ikiwemo kuuza miili yao.

Kwa mujibu wa utafiti wa viashiria vya Ukimwi wa mwaka 2016/17 unaonyesha vijana 90 kati ya watu 225 hupata maambukizi mapya kila siku na kati ya vijana hao mabinti ni 72.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Septemba 11, 2019 katika mkutano wa mwaka wa vijana balehe na wanawake vijana kupitia mradi wa ‘Dreams’ uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ulifadhiliwa na shirika linaloshughulikia watoto duniani (Unicef), Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na kuratibiwa na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) huku ukitekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Shinyanga, Kagera na Mbeya.

Akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Tacaids, Jumanne Isango amesema kundi hilo hukabiliwa na changamoto nyingi ambazo ni vigumu kupambana nazo ikiwa hakuna namna ya kuwapatia elimu juu ya namna ya kuepuka mazingira hayo.

“Mkutano huu unatufanya sisi kutambua kwa undani ili wadau wanapoondoka hapa wajue tunaimarisha vipi mradi wetu huu au tunatakiwa kufikia mikoa gani mingine ambapo mradi huu unahitajika zaidi,” amesema Isango

Advertisement

 

Mradi huo umekuwa ukitoa elimu kwa mabinti ili wajitambue na kuondokana na matumizi ya njia hatarishi kupata fedha huku mabinti 2,300 kutoka halmashauri 11 nchini humo wakiwa tayari wamefikiwa na elimu hiyo tangu kuanza kwa utekelezaji wake miaka miwili iliyopita.

Mchumi Mkuu kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Sauda Aman amesema ili kufikia wasichana walio katika hali duni za kimaisha wamekuwa wakiwatumia maofisa jamii kutoka halmashauri mbalimbali walio katika maeneo yao.

“Wanaangalia wale ambao wako katika hali duni, anajua huyu anaishi na bibi anapaswa kufikiwa na mradi huo,” amesema Sauda

Advertisement