VIDEO: Umasikini watajwa kupungua Tanzania

Naibu Waziri wa fedha na Mipango Dk Ashatu Kijaji akijibu maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema umasikini nchini umepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema umasikini nchini umepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Septemba 11, 2019 na naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji bungeni mjini Dodoma.

Dk Kijaji amesema mwaka 2012 umasikini Tanzania ulikuwa  asilimia 28.2 lakini mwaka 2018 umekuwa asilimia 26.8, kwamba  katika kipindi hicho umasikini wa chakula umepungua kutoka asilimia 9.7 kufikia asilimia 4.4 mwaka, 2018.

Katika swali la nyongeza mbunge wa Bunda (CCM), Mwita Getere amehoji lini Serikali itaondoa umasikini baada ya kuonyesha mafanikio katika maradhi na ujinga.

"Si kweli kuwa umasikini haupungui bali umepungua na unaendelea kupungua kwa kiasi kikubwa, na hii ni taarifa ya kisomi kutoka kwa watu maalumu," amesema Dk Kijaji.

Kuhusu kudhibiti kasi ya ongezeko la ukuaji wa idadi ya watu, Dk Kijaji amesema ongezeko la watu ni fursa kwa nchi ikiwa fursa zitatumiwa ipasavyo.