Umoja wa mabunge duniani wazungumzia kilio cha Lissu, wengine

Muktasari:

Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kupitia kamati yake ya Haki za Binadamu  imetoa maamuzi juu ya malalamiko ya Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu.

Moshi. Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kupitia kamati yake ya Haki za Binadamu  imetoa maamuzi juu ya malalamiko ya Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu.

Pia, IPU imetoa maamuzi ya malalamiko ya wabunge katika nchi mbalimbali duniani na Afrika Mashariki, malalamiko ya Lissu yamepewa uzito mkubwa.

Lissu aliwasilisha malalamiko sita yaliyohusu ukiukwaji wa haki za binadamu, vitisho na kukamatwa na kuwekwa kizuizini.

Makamu mwenyekiti huyo wa Chadema alilalamikia kutokuwepo kwa mwenendo wa haki wa vikao vya Bunge la Tanzania, kuminywa uhuru wa kutoa maoni na kujieleza na kukuikwa kwa haki ya mikusanyiko.

Lissu alieleza  kuwa Septemba 7, 2017 alinusurika kifo katika jaribio la kumuua lililofanywa na watu waliokuwa na bunduki aina ya AK-47 katika makazi yake jijini Dodoma.

Kamati hiyo ya IPU imesema mlalamikaji (Lissu) alieleza kuwa tukio hilo lilitokea katika nyumba za Serikali ambazo alikuwa anaishi na zenye ulinzi mkali, lakini siku hiyo walinzi hawakuwepo.

Kamati hiyo pia imeeleza  namna Lissu alivyovuliwa ubunge wake isivyo halali Juni 2019 kutokana na kutokuwepo bungeni, wakati ikijulikana wazi kwa umma kuwa alikuwa nje ya nchi kwa matibabu.

“Alieleza (Lissu) kuwa Spika wa Bunge la Tanzania na Naibu Spika na baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Tanzania ndio waliofanya uamuzi wa kumpakia kwenye ndege kwenda Kenya kwa matibabu,” inaeleza kamati hiyo.

Kamati ya Haki za Binadamu ya IPU imekubali kuwa malalamiko ya Lissu yanakubalika chini ya kanuni za uchunguzi na uamuzi wa malalamiko za IPU na ina mamlaka ya kuchunguza.

Kamati hiyo imeeleza kusikitishwa kwake na jaribio la mauaji dhidi ya Lissu na tuhuma za kuhusika kwa mamlaka za Serikali katika jaribio hilo ambalo imesema Lissu alinusurika kimiujiza.

Kamati hiyo imesema ni jambo linalotatiza kwamba Lissu alivuliwa ubunge wake wakati ilikuwa wazi kwa Bunge na umma kwamba Lissu alikuwa nje ya matibabu kutokana na shambulio hilo.

“Kamati inapongeza hatua za haraka zilizochukuliwa kumpeleka eneo salama na kuhakikisha anapata matibabu lakini inataka kujua Bunge lilichukua hatua gani kufuatilia uchunguzi,” inasema.

Kamati hiyo imeeleza kuwa inapenda kupata maoni kutoka kwa Mamlaka ya Bunge la Tanzania kuhusu sababu za Lissu kuvuliwa ubunge.

Kamati hiyo inataka kupata taarifa rasmi kutoka Serikali ya Tanzania kuhusu ukweli na uhalali wa kisheria kuhusu kila hatua inayohusu kukamatwa kwake na kushtakiwa mahakamani.

Lakini kamati hiyo ya IPU imesema inatambua Lissu anataka kurejea Tanzania haraka, imeshauri kuundwe  kamati ndogo ambayo itamsindikiza hadi Tanzania siku akirejea.

“Kamati inaamini kuwa kuzuru Tanzania kutatoa fursa muhimu kukutana na Serikali, Bunge na Mahakama au mtu yeyote ambaye atasaidia kutoa uelewa wa suala hilo la kurejea kwa Lissu.

Kamati imemuomba Katibu Mkuu wa IPU kuwasilisha uamuzi huo kwa mamlaka ya kibunge ya Tanzania na kuomba ruhusa ya kutembelea Tanzania kama ilivyopendekezwa.

Pia Kamati itaendelea na uchunguzi wa malalamiko haya katika kikao chake kijacho.

Kufuatia uamuzi huo, jana Jumanne Februari4, 2020 Lissu alisema amefurahishwa na uamuzi wa kamati hiyo kuchunguza maamuzi ya kuwafukuza au kuwasimamisha Wabunge kuhudhuria vikao vya Bunge.

“Ushauri wangu ni kwamba Wabunge wetu wote ambao wameathiriwa na vitendo hivi wawasilishe malalamiko yao kwa IPU ili yachunguzwe.”

“Mtaona kwenye taarifa hii (ya kamati ya IPU) jinsi ambavyo malalamiko kutoka sehemu mbali mbali duniani, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, yameshughulikiwa,” amesema.

Lissu amesema kufanya hivyo kutaongeza shinikizo kwa watawala na uongozi wa Bunge ili angalau vyombo hivyo na wananchi wajue vitendo vya ukiukaji haki za wabunge vinamulikwa duniani.