Fahamu yaliyojiri leo mahakamani kuhusu kesi ya kutekwa Mohamed Dewji 'Mo'

Mtuhumiwa wa Kesi ya kumteka mfanyabiashara mohamedi  dewji Dereva Mouse Twaleb akipandisha kusomewa mashtaka  yake  katika mahakamani Kisutu. Picha na Omar Fungo

Dar es Salaam. Wakili wa Utetezi,  Robert Mtakula ameuomba upande wa mashtaka kuongeza jitihada za kuwatafuta washtakiwa watano  wanaodaiwa kumteka mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo’ ili waunganishwe na Mousa Twaleb.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Septemba 16, 2019 baada ya wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon kudai mbele ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa ilitolewa hati ya kukamatwa kwa washtakiwa hao, wanaendelea kuwatafuta na wataeleza mahakama walipofikia.

SOMA ZAIDI

Mahakama imeshatoa hati ya kukamatwa kwa Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior (wote raia wa Msumbiji) na Phila Tshabalala,  raia  wa Afrika Kusini.

Twaleb, mkazi wa Tegeta tayari alishafikishwa mahakamani na  kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Mtakula amedai hati ya kukamatwa kwa washtakiwa hao ilishatolewa na mahakama, “Ninaomba jitihada zifanywe ili kuhakikisha wanakamatwa na  shauri liweze kuendelea mbele.”

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 30, 2019.

Washtakiwa hao wakikamatwa wataunganishwa katika kesi hiyo kujibu mashitaka mawili ya  kumteka nyara Mo kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari na kuongoza genge la uhalifu.

Inadaiwa Mei Mosi, 2018 na Oktoba 10, 2018 katika jijini Dar es Salaam na Johannesburg, Afrika Kusini kwa makusudi washitakiwa wote kwa pamoja waliendesha genge la uhalifu.

Pia inadaiwa Oktoba 11, 2018  maeneo ya  Hoteli ya Colloseum  wilayani Kinondoni Dar es Salaam, Twaleb pamoja na watu wengine  walimteka Mo kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.

Inadaiwa Julai 10, 2018 maeneo ya Mbezi Beach wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb alitakatisha fedha  Sh8 milioni wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.

Mo alitekwa  Oktoba 11, 2018 alfajiri  katika hoteli hiyo wakati akienda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, 2018  katika eneo la Gymkhana.

SOMA ZAIDI